Hongera NIDA, kazi bado kubwa

Maoni ya Katuni.
Jana Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ilitoa vitambulisho vya kwanza 46 kwa watu mbalimbali wakiwamo viongozi wakuu wa kitaifa walioko madarakani na waliokwisha kustaafu.

Hizi ni hatua za awali kabisa katika safari na kazi kubwa na ngumu ya kutoa vitambulisho vya taifa kwa kila mwananchi.

Ni jambo la kufurahisha kwamba kazi hii ambayo kwa miaka mingi ilikuwa kama simulizi isiyotimia, imeanza kuzaa matunda, na sherehe za uzinduzi wa utoaji vitambulisho zilionyeshwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya televisheni nchini zikihudhuriwa na Rais ambaye amekuwa wa kwanza kupewa kitambulisho hicho, akifuatiwa na mkewe na marais wastaafu wa awamu ya pili na tatu.

Pia viongozi wengine kadhaa wakiwamo wa vyama vya upinzani nao walipewa vitambulisho hivyo.

Tanzania sasa inaingia katika historia mpya ya kuwa na vitambulisho vya uraia tangu nchi hii ipate uhuru mwaka 1961. Tunaipongeza Nida kwa hatua zilizopigwa na mafanikio haya makubwa.

Tunajua kuwa kazi hii ni kubwa kama tulivyokwisha kueleza hapo juu, hata hivyo ni matarajio ya Watanzania kwa ujumla wao kwamba kazi hii itafanywa kwa uadilifu mkubwa ili wale watakaopata vitambulisho kweli wawe ni wenye haki ya kupewa.

Tunasema haya kwa kuwa hata wakati Rais anatoa hotuba yake katika serehe za kukabidhi vitambulisho jana alitoa hadhari kwamba mchakato wa kutoa vitambulisho vya taifa usijekuwa kama ule wa kutoa pasi za kusafiria za Tanzania ambazo zimekuwa zikitolewa kwa watu wasiostahili.

Hili limekuwako kwa miaka mingi na kwa bahati mbaya sana limechafua jina zuri la taifa letu kwa wenye pasi hizo kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama usafishaji wa dawa za kulevya.

Kwa maana hii, Nida ni lazima wajue kwamba sasa wanaingia katika ngazi ngumu zaidi ya kuendesha mchakato wa kutoa vitambulisho vya taifa kwa kuanza kuhakiki majina ya waliokwisha kujaza fomu, lakini pia kuendesha mchakato huo nchi nzima. Hii siyo kazi ndogo, inahitaji kujituma, uvumilivu lakini la muhimu zaidi uadilifu.

Katika nchi za Kiafrika ambazo mipaka ilibuniwa tu na wakoloni baada ya kukaa kule Berlin mwaka 1884-1885, ni kawaida kabisa kabila moja kukatwa mara mbili hivyo kuwa katika nchi mbili tofauti.

Kuna makabila kama Wamasai ambao wako Kenya na Tanzania, kuna Waha ambao hawatofautiana na Warundi, wapo Wajaluo Kenya na Tanzania, wapo Wakurya wa Kenya na Tanzania, wapo Wamakonde wa Tanzania na Msumbiji, kwa kifupi makabila mengi ya mipakani yametanda nchi mbili.

Hawa ni ndugu, wanaendeleza undugu ndiyo maana kwa mfano mila zao zinadumishwa kwa pamoja kama kuwa na chifu mmoja, matambiko ya pamoja na vitu kama hivyo.

Katika mazingira kama hayo hakika Nida itakuwa na kibarua kizito na kigumu kujua ni yupi katika maeneo kama haya anastahili kupata kitambulisho na yupi hastahili kwa maana ya uraia wa kila mmoja.

Tunafikiri maeneo kama haya umakini unastahili kuchukua nafasi yake, vyombo mbalimbali vya usalama vinapaswa kushiriki, lakini zaidi sana wananchi ambao ni wakazi wa maeneo husika wanapaswa pia kusaidia kazi hii ili iwe ya manufaa kwa taifa hili.

Tunapoingia katika mchakato huu wa kupata vitambulisho vya taifa ni vema wananchi wakajua kuwa huu ni mradi mkubwa wa kwanza kufanywa na nchi hii kwa maana ya kujaribu kujenga mifumo ambayo itatusadia kama wananchi na taifa kufanya mambo yetu kwa ufanisi.

Kama Nida itatimiza wajibu wake sawasawa na kwa kusaidiwa sana na ushirikiano wa wananchi, itasaidia kuondoa vikwazo vingi vya kujuana na kutekeza jukumu na kusaidia mifumo mingi kufanya kazi vizuri. Kujuana ni jambo la maana sana katika taifa lolote; zipo faida nyingi za kujua huyu ni nani na yuko wapi, mojawapo ya faida zake ni kutambuliwa hata na taasisi za fedha, kuaminika na kupata fursa ya kufanya shughuli za kiuchumi na taasisi hizi.

Tunapongeza kazi ambayo tayari imekwisha kuanza kufanywa na Nida na matokeo ambayo yameonekana jana kwa kutolewa vitambulisho vya taifa, sasa tunawatakia kila la kheri katika safari yao ndefu, ngumu na yenye changamoto nyingi ya uwajibikaji ili kweli ifikapoi mwaka 2015 kila mwananchi mwenye sifa ya kupewa kitambulisho chake awe amekipata na wale wenye sifa ya kupigakura kweli wavitumie katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company