Maoni ya Katuni
Tatizo la maji limekuwa sugu katika miji na vitongoji vingi hapa nchini, baadhi ya taasisi na Mashirika makubwa yaonekana kujiingiza katika mchakato wa kuimarisha huduma ya maji katika maeneo mengi ya mijini na vijijini.
Hata hivyo, bado jitihada kubwa zinatakiwa kufanywa na watafiti kutoka taasisi za elimu ili kumaliza kabisa tatizo la maji nchini.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewataka watafiti na wanasayansi nchini kulitafutia ufumbuzi tatizo la maji ambalo husababisha magonjwa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na homa ya matumbo pamoja na kipindupindu kwa rika zote za wananchi.
Wito huu aliutoa hivi karibuni wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa wanasayansi pamoja na watafiti wa maji kutoka Barani Afrika na nchi mbalimbali duniani, ulioandaliwa na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela jijini Arusha.
Waziri Mkuu akasema tatizo la maji bado ni kubwa jambo ambalo husababisha madhara mbalimbali ikiwemo homa ya matumbo kwa watoto wadogo.
Suala la maji ni changamoto kwa kila nchi na pia wanasayansi pamoja na watafiti wanatakiwa kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha maji yanatunzwa kwa lengo la kuzuia maambukizi yakiwemo magonjwa ya kuhara.
Athari za magonjwa ya aina hiyo zimejidhihirisha katika maeneo mengi nchini ikiwa ni pamoja na katika miji mikubwa kama Dar es Salaam ambako kila wakati hutokea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu akabainisha kuwa Tanzania kupitia Wizara ya Maji imeanza kufanya jitihada ambapo hivi sasa lipo ongezeko la maji katika maeneo ya vijijini na mijini kunakotokana na wananchi kuhamasishwa juu ya utunzaji wa mazingira pamoja kutokata miti ovyo na kuchoma misitu.
Ingawa ni ikweli kwamba Tanzania inajitahidi kuhakikisha tatizo la maji linaisha lakini changamoto ni kubwa hasa katika kutunza vyanzo vya maji, na ndio maana wataalamu wanakutana ili kuzijadili kuhakikisha maji yanapatikana kwa wingi kwani maji ni uhai na maisha lazima yaendelee.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu ni muhimu sana kuzingatiwa kwani jitihada zinazofanywa na serikali kutokana na uhaba wa maji safi ni kwa ajili ya kuokoa maisha ya Watanzania wote walioko mijini na vijijini.
Mkutano huo wa watafiti ulikuwa ni muhimu na tunaamini kwamba mengi yaliyojadiliwa yalionyesha uzoefu wa nchini mbalimali jinsi zinavyokabiliana na utatuzi wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wake.
Suala la upatikanaji wa maji safi na salama na hata udhibiti wa maji taka limepigiwa kelele na wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa. Kwa mfano, katika kikao cha Bunge kilichomalizika wiki hii, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika aliwasilisha hoja binafsi kuhusu uhaba wa maji akitolea mfano Jiji la Dar es Salaam.
Akasema maji ni uhai, hivyo matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na nchini kwa ujumla kama hatua za haraka zisipochukuliwa yatageuka kuwa janga la taifa.
Katika kila watanzania katika Jiji la Dar es Salaam na nchini; kwa wastani mmoja hapati huduma ya maji safi na salama na hali ni mbaya zaidi kuhusu ushughulikiaji wa maji taka, aliongeza kusema.
Ingawa hoja yake haikuwepa nafasi katika mjadala wa Bunge, lakini hoja yake ilikuwa ya msingi hasa ikizingatiwa kwamba uhaba wa maji katika maeneo mengi ni dhahiri, hivyo jitihada za ziada za mamlaka husika zinatakiwa ili kuepusha madhara zaidi kwa wananchi.
Ni imani yetu kwamba mkutano ule wa watafiti ambao wataalamu wetu pia walishiriki, watalifanyia kazi tatizo la maji nchini ili kupata suluhisho la kudumu kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na huduma bora kushughulikia maji taka.
Kama Mkuu wa Chuo cha Nelson Mandela, Profesa Burton Mwamila alivyosema katika mkutano huo kwamba chuo hicho kwa kushirikiana na vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi wataendelea kutafiti masuala mbalimbali yanayohusu jamii ikiwemo masuala ya afya na teknolojia ili kuweza kuendana na mabadiliko ya tabia nchi.
Tafiti zitakazofanyika zihusishe maeneo ya kusambazia maji kwa walengwa, uzoefu umeonyesha kuwa hata yale maji machache yaliyopo, mengi hupotelea njiani kutokana na miundombinu yake kuwa chakavu.
Isitoshe, wakati mwingine maji hupotea kutokana na wananchi wengi kujenga makazi maeneo yasiyopimwa, matokeo yake wananchi hao huyakata mabomba hayo kwa makusudi ya kujigemea maji isivyo halali. Inaonekana nchi hii ina vyanzo vingi vya maji ambayo hupotea bure katika msimu wote wa mwaka. Ni wakati muafaka sasa kwa serikali kuwekeza kwa nguvu kubwa katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kuhifadhi maji hayo. Pia ujenzi wa makazi uzingatie mipango miji ili kuepusha adha na upotevu wa maji usiokuwa wa lazima