KAIMU Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo, anashikiliwa na polisi kwa siku ya tatu leo, akihusishwa na tukio la kumwagiwa tindikali, Musa Tesha.
Tesha alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana Septemba 9, mwaka juzi kwenye kampeni ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, uliomuweka madarakani Dk. Kafumu Dalali.
Akizungumza juzi na Tanzania Daima kabla ya kufika makao makuu ya Jeshi la Polisi, Kilewo alisema hajui anachoitiwa na kwamba anatekeleza wito wa jeshi hilo kuwa afike ofisini kwao.
“Sijui ninachoitiwa, nimepigiwa simu naenda kutekeleza wito, nimesha wataarifu mawakili wangu ninaowaamini, kwa kuwa chochote kinaweza kutokea cha msingi Watanzania wapenda mageuzi waniombee kwa Mungu,” alisema Kilewo.
Wakili wa Kilewo, Peter Kibatala, alisema baada ya mteja wake kuhojiwa kwa muda wa saa tano juzi alielezwa kuwa anapelekwa Igunga, mkoani Tabora kuunganishwa na watuhumiwa wengine katika kesi ya kutumia tindikali na kujeruhi.
Kibatala alisema anasikitishwa na hatua ya jeshi hilo kumnyima dhamana mteja wake ilhali kosa wanalomtuhumu linadhaminika na kwamba hayo ni matumizi mabaya ya madaraka kumzuia mtu kwa zaidi ya saa 24 pasipo kumfikisha mahakamani.
Wengine wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutumia tindikali na kudhuru watu ni pamoja na Oscar Kaijage wa Shinyanga na Evodius Justinian wa Bukoba.
Evodius Justinian alikamatwa na Jeshi la Polisi mjini Bukoba na kushikiliwa kwa siku kadhaa kabla ya kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kusafirishwa na kufikishwa jijini Da r es Salaam, Justinian alieleza kuteswa na kupigwa na askari waliokuwa wakimzuia katika vituo mbalimbali kuanzia mjini Bukoba.