Melema akiwa mahakamani
Mwanasiasa wa upinzani nchini Afrika Kusini, Julius Malema ameshindwa katika juhudi zake za kutaka kesi ya ufisadi dhidi yake itupiliwe mbali huku akikabiliwa na tisho la kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo mwaka ujao.
Kiongozi huyo wa zamani wa tawi la vijana la chama tawala ANC ameshitakiwa kwa makosa ya kutengeza pesa kwa njia haramu , udanganyifu na kujihusisha na mitandao ya uhalifu.
Jaji Ephraim Makgoba alisema kuwa kesi itaanza kusikilizwa tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 2014.
Anadaiwa kupokea dola za kimarekani, 392,000 kutokana na mikataba na maafisa wa serikali , madai anayoyakanusha.
Mamia ya wafuasi wa chama kipya cha Malema, (Economic Freedom Fighters), walikusanyika katika mahakama kuu ya Polokwane mjini Limpopo kusikiliza uamuzi wa jaji.
Wafuasi hao waliokuwa wamebeba vuvuzela na virungu, waliimba nyimbo za kumpinga Rais Jacob Zuma.
Jaji alisema kuwa Melema atafikishwa mahakamani pamoja na washtakiwa wenza wanne hadi labda kiongozi wa mashitaka atakapoamua kumwondolea kesi hio.
Serikali inadai kuwa Malema na wenzake wajiwakilisha ili waweze kupata kandarasi ya serikali ya thamani ya dola milioni 5.
Lakini Malema anasema kuwa mashitaka dhidi yake ni njama ya kisiasa kumponza.
Kucheleweshwa kwa kesi hiyo ina maana kuwa Melema hatajihusisha na kampeini za uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Malema anasema ikiwa atachaguliwa atahakikisha kuwa mali ya Afrika Kusini itawafikia watu masikini na vijana wengi wasio na ajira wamevutiwa zaidi ya wito huu.
Alifurushwa kutoka chama tawala ANC mwaka 2012 kwa madai ya kuchochea migawanyiko chamani.