Waandishi walioripoti kuhusu taarifa ya mwanamke huyo kubakwa wamepewa kifungo cha nje
Mahakama nchini Somalia, imemhukumu kifungo cha nyumbani mwanamke aliyedai kubakwa pamoja na waandishi wawili wa habari waliomhoji kuhusiana na madai hayo.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 19, alipewa kifungo cha nje cha miezi sita kwa kile mahakama ilisema ni kutoa taarifa zisizokweli.
Atalazimika kukaa nyumbani kwake bila kutoka nje kwa miezi sita.
Mmoja wa waandishi wa habari, aliyemhoji mwanamke huyo naye alipewa kifungo cha nje cha mwaka mmoja huku mwenzake akipokea kifungo cha miezi sita.
Waandishi hao wanafanya kazi na kituo cha redio Shabelle ambacho serikali ilifunga matangazo yake mwezi Oktoba baada ya polisi kuvamia ofisi zake.