EMBU SOMA TENA MAKALA HII ILIYO ANDIKWA NA PRO SHIFJI 25/12/2013,RAIA MWEMA;"Haina maana waziri mkuu kung’olewa"



AIBU, aibu, aibu. ... aibu ya kitaifa! Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili uliosababisha mateso, ukatili, udhalilishwaji, upigaji na hatimaye vifo vya wananchi ni aibu kubwa kwa taifa letu. Sio aibu tu bali ni janga la kitaifa linalohitaji kufanyiwa tathmini na tafakuri na wananchi wote katika ujumla wao na kujiuliza: tunaelekea wapi? Nini kimesababisha vyombo vya dola na mfumo wetu wa kisiasa kukosa kabisa uwajibikaji kiasi kwamba vyombo vilivyopewa jukumu la kuyalinda maisha, utu na heshima ya wananchi, vigeuke kuwa watesaji na wadhalilishaji wa wananchi hao hao! Kwa nini hatujifunzi? Kwa nini hatujirekebishi?
Operesheni Tokomeza Ujangili
Katika historia yetu tumewahi kuwa na janga kama hili mwaka wa 1976 kutokana na Operesheni Mauaji huko Shinyanga na Mwanza. Mwalimu Nyerere aliwalazimisha viongozi wa kisiasa, akiwamo Mzee Mwinyi, kujiuzulu na watendaji wengine, wakiwemo wakuu wa Jeshi la Polisi na usalama katika ngazi ya mkoa, kuchukuliwa hatua za kisheria na kuadhibiwa ipasavyo. Tukio la Operesheni Tokomeza linafanana na tukio la Operesheni Mauaji, lina sura ile ile ya utesaji, udhalilishaji, ubakaji na uporaji wa mali ya wananchi.

Matukio mengine ya aina hiyo, japokuwa hayakuwa makubwa kiasi hicho, yamewahi kutokea huko nyuma. Katika awamu ya pili, kulikuwa na mauaji ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero mwaka 1986, na madhara na mateso waliyoyapata wananchi wakati wa Mwembechai. Katika awamu ya tatu ilitokea kashfa ya waandamaji huko Pemba kuuawa na wengine kudhalilishwa kiasi kwamba tukio hili lilileta aibu kubwa kwa taifa. Kwa jumla, matukio kama haya, yaani utumiaji wa mabavu na vyombo vya mabavu – polisi, usalama, maaskari wengine kama wanamgambo na askari wa wanyama pori – yameongezeka awamu hadi awamu kiasi kwamba katika awamu ya nne tunashuhudia mauaji na mateso ya wanahabari na wananchi yakiongezeka mara dufu. Hili la Operesheni Tokomeza ni kilele.

Sasa tufanyeje?

Kwanza uwajibikaji

Mawaziri wanne wamelazimishwa kuachia ngazi kwa kubeba dhamana ya kisiasa. Na wamepongezwa! Mengi mengine yanazungumziwa kwa mtazamo wa kichama na kisiasa. Wengine wanaenda mbali kusema kwamba Waziri Mkuu pia anatakiwa kujiuzulu. Haya yanaeleweka kwa sababu tukio lenyewe limeamsha hisia za watu na watu wanataka kuona waziwazi kwamba hatua za maana zinachukuliwa kuwatuliza.

Ni kweli kabisa kwamba tukio hili ni kashfa kubwa sana ya kitaifa. Katika mfumo wa kibunge (parliamentary system), serikali nzima pamoja na mkuu wa serikali, yaani waziri mkuu, wangejiuzulu na labda Uchaguzi Mkuu ungeitishwa. Lakini katika mfumo wetu wa urais (presidential system), mkuu wa serikali sio Waziri Mkuu. Ni rais, na rais pia ni mkuu wa nchi. Kwa hivyo, kujiuzulu kwa Waziri Mkuu hakuna uzito. Kwa upande mwingine, huwezi kutegemea rais mwenyewe na serikali yake kujiuzulu kwa sababu, rais pia ni mkuu wa nchi. Na huwezi ukawa nchi bila kiongozi mkuu; kutakuwa na ombwe la uongozi.

Kwa upande wangu, ili kuonyesha kwamba tukio hili linachukuliwa kwa uzito wake, na hisia za wananchi zinajibiwa ipasavyo, mambo mawili yafuatayo yanaweza kufanyika mara moja:

Moja, Rais kuvunja Baraza lake lote la Mawaziri, kama alivyofanya Mzee Mwinyi miaka ya tisini. Hatua hii itakaribiana na uvunjaji wa serikali. Hii itakuwa ni dalili ya uwajibikaji wa kisiasa.

Pili, watendaji, wakiwemo wale katika ngazi za juu, wafikishwe mbele ya Mahakama kwa mashtaka ya kijinai. Mwanasheria Mkuu amependekeza uundaji wa Tume ya Kimahakama. Hii ni njia mojawapo lakini mara nyingi njia hii hutumika kama mbinu za kufunika kombe ili mwanaharamu apite. Nionavyo, labda safari hii, Rais Kikwete anaweza kutumia njia mbadala ya kuteua mchunguzi huru (independent investigator and prosecutor) ambaye atakusanya ushahidi na kuandaa mashtaka ya kupeleka mbele ya Mahakama.

Na katika uchunguzi huu, watendaji wote wanaohusika, pamoja na wa kijeshi, usalama, na wa kiraia, wachunguzwe na kushtakiwa bila kujali nyadhifa zao.

Tatu, jambo hili lizungumzwe na kujadiliwa na taifa zima kwa upana na undani wake bila kuficha au kulionea haya. Hakuna shule muhimu ya kujifunza kuliko shule ya umma. Shule ya umma inafundisha na pia inasaidia kujenga maadili na uwajibikaji. Katika mijadala idara zitatajwa, watu waovu watasemwa kwa majina, maovu yanayofichwa uvunguni yatafichuliwa hadharani.

Mwishowe, ningependa kuligusia jambo moja muhimu ambalo linaonekana halijaguswa hata kidogo.

Dola na matumizi ya mabavu

Dola ni taasisi ya mabavu, popote pale duniani. Jeshi, Polisi, maaskari wengine kama wa wanyamapori, wa hifadhi na kadhalika ni vyombo vya mabavu. Vyombo hivyo vya mabavu katika dola vinapata uhalali wa kisiasa kutumia mabavu kwa sababu vinadhibitiwa na kusimamiwa na vyombo na viongozi wa kisiasa ambao hupata uhalali wao kutokana na kuwa wawakilishi wa wananchi. Kwa mfano, Jeshi la Ulinzi hutumia mabavu kuilinda nchi dhidi ya maadui wa nje. Uwezo wa kutangaza vita na kuingiza jeshi vitani ni wa Rais kama Amiri Jeshi Mkuu; na rais ni kiongozi wa kisiasa aliyechaguliwa, sio mwanajeshi.

Katika mfumo wowote ule ambao ni wa kiraia, kwa maana kuwa sio wa kijeshi (military) au wa kipolisi (police state), vyombo vya kisiasa ndio hudhibiti na kusimamia vyombo vya mabavu. Jukumu la jeshi la ulinzi ni kuilinda nchi. Jukumu la jeshi la polisi ni kulinda amani, wananchi na mali zao. Majukumu haya mawili ni tofauti na yanatenganishwa kikatiba. Hayaingiliani.

Ndio maana, jeshi la ulinzi halitumiki kudhibiti ghasia nchini. Hii ni kazi ya polisi. Katika mazingira ya kipekee ambayo kuna hatari ya serikali kupinduliwa kwa nguvu au kama kuna uasi ndio Jeshi la Ulinzi huingizwa mitaani. Na jambo hili hufanyika baada ya Rais kutangaza hali ya hatari kwa mujibu wa masharti ya katiba.

Kwa hivyo, ni kinyume cha Katiba na mazoea mabaya kuliingiza jeshi la ulinzi katika mambo ya kiraia, kama vile uhalifu au ujangili. Kufanya hivyo ni kujenga mazoea mabaya na ya hatari sana.

Kinyume cha msingi huu wa kikatiba, Operesheni Tokomeza ilichukuliwa kama operesheni ya kijeshi. Katika washiriki 2,371, wanajeshi walikuwa 885 au asilimia 37, yaani zaidi ya theluthi moja. Polisi walikuwa 480 au asilimia 20 tu. Wengine walikuwa kutoka majeshi mbalimbali kama la wanyapori n.k.

Pili, operesheni hii ilisimamiwa na Jeshi la Ulinzi. Na nikinukuu maneno ya Taarifa ya Kamati ya Bunge, “Taarifa za mwenendo wa operesheni zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja kwa Mkuu wa Majeshi na kwamba, hazikumfikia Waziri wa Maliasili na Utalii.” Isitoshe, viongozi wa kisiasa kama wakuu wa wilaya na mikoa na viongozi wa kuchaguliwa kama madiwani, hawakushirikishwa wala hawakupewa taarifa zozote kuhusu operesheni hii. Mbaya zaidi, baadhi yao waliteswa na kudhalilishwa na maaskari waliohusika na operesheni kiasi kwamba Mkuu wa Wilaya ya Ulanga alijificha katika hoteli.

Kwa kifupi basi, operesheni hii haikudhibitiwa wala kusimamiwa wala kuendeshwa kama operesheni ya kiraia (civilian operation), badala yake iliendeshwa kama operesheni ya kijeshi (military operation). Hili ni jambo la hatari sana na ni mazoea mabaya, hayakubaliki katika mfumo wa utawala wa kiraia (civilian government).

Kuchanganya jeshi la ulinzi na mambo ya kiraia ni dhambi kubwa katika mfumo wa kisiasa tunaoufuata nchini mwetu. Jambo hili halikubaliki kabisa!.

Kwa hivyo, inashangaza kwamba hata Kamati ya Bunge haikuona hili na badala yake ikapendekeza kwamba Serikali iandaae “operesheni nyingine ambayo itapangwa na kutekelezwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Idara ya Usalama wa Taifa. ” Na hoja hii inaonekana kuungwa mkono bila kutiliwa shaka na wabunge wetu! Maana yake nini, wabunge hawajui na hawatambui kwa kuruhusu hili wanajenga mazoea hatari? Kama ndivyo basi ipo haja ya wanasiasa wetu pamoja na wabunge kujielimisha zaidi jinsi serikali za kiraia zilizochaguliwa na wananchi zinavyoendeshwa.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company