WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Dk. William Augustao Mgimwa (63) amefariki dunia.
Waziri huyo katika Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete amefariki dunia jana baada ya kuugua kwa muda mrefu na kulazwa katika Hospitali ya binafsi ya Milpark nchini Afrika Kusini.
Kutokana na kifo hicho, Rais Kikwete amesema amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri Mgimwa, aliyekuwa pia Mbunge wa Kalenga (Mkoa wa Iringa) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi alisema taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi hiki ambacho alikuwa anahitajika zaidi kutokana na mchango wake mkubwa aliokuwa akiutoa kupitia nafasi zake za waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, kifo cha Waziri Mgimwa kilitangazwa jana mchana, Januari mosi, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika tangazo lake, Balozi Sefue alisema Waziri Mgimwa ameaga dunia jana majira ya saa 5:20 asubuhi (saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini ambako amekuwa amelazwa kwa muda sasa.
Balozi Sefue alisema maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri Mgimwa yanafanywa na serikali kwa kushirikiana na familia yake na kuwa taarifa zaidi zitatolewa baadaye kwa kadiri zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.
Katika salamu zake kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na kwa familia ya marehemu Mgimwa, Rais Kikwete alisema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha Mheshimiwa Mgimwa. Binafsi nimemtembelea mara mbili kwenye Hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.”
Rais Kikwete aliendelea kusema: “Sote tunajua mchango wake katika serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”
“Napenda kutoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” amesema Rais Kikwete.
Rais pia amewatumia rambirambi wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa wamempoteza mwakilishi na mtetezi mahiri wa masilahi yao.
Mgimwa aliyezaliwa Januari 20, 1950 na kuwa mbunge wa Kalenga mkoani Iringa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), anadaiwa alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo.
Hata hivyo, hakuna aliyekuwa tayari kueleza ni ugonjwa gani ambao unamsumbua msomi huyo wa masuala ya uchumi, ambaye alianza kuwa waziri miaka miwili iliyopita.
Hali ya waziri huyo iliripotiwa kuwa mbaya kuanzia mwanzoni mwa Desemba mwaka jana na baadaye ilianza kuimarika taratibu tangu alipolazwa katika Hospitali ya Milpark nchini humo.
Kifo cha Waziri Mgimwa kinazidi kuongeza pengo la mawaziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ambaye sasa atakuwa anakuna kichwa kumpata mrithi wa waziri huyo wa Fedha na Uchumi.
Hivi sasa Rais Kikwete anatarajia kuziba pengo la mawaziri wanne waliong’olewa kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Mawaziri hao na wizara zao kwenye mabano ni David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Pia kama Rais Kikwete atakubali kutekeleza mapendekezo ya chama chake ya kutaka awatose mawaziri mizigo, atakuwa na wakati mgumu zaidi wa kujaza nafasi ya mawaziri zaidi saba wanaoangukia katika kundi la mawaziri mizigo.
Dk. Mgimwa alikuwa mkufunzi katika Chuo cha Benki Kuu mkoani Mwanza, kabla ya kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mkoa wa Iringa, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Mgimwa alizaliwa Januari 20, mwaka 1950.
Alipata Shahada ya Uzamili ya masuala ya fedha katika Chuo Kikuu cha Mzumbe kati ya mwaka 1989-1991.
Alisoma ‘Postgraduate Diploma’ ya masuala la fedha katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kati ya mwaka 1983-1984 na Stashahada ya masuala ya benki katika Chuo cha IFM kati ya mwaka 1975-1978.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, alisoma Shule ya Tosamaganga kati ya mwaka 1968-1969 na baadaye Shule ya Sekondari Mafinga.
Kabla ya kuwa mbunge, amewahi kufanya kazi katika Benki ya NBC katika nyadhifa mbalimbali kati ya mwaka 1980 hadi 2000.
