Serikali tatu zaigawa CCM, CUF

UWEZEKANO wa Katiba ya zamani ya Tanzania ya mwaka 1977 kuendelea kutumika umeanza kujitokeza baada ya vyama vikuu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), kutofautiana kimsimamo kuhusu rasimu ya pili ya Katiba inayopendekeza mfumo wa serikali tatu.

Hali hiyo imejitokeza visiwani humu siku moja tu baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukabidhi rasimu ya pili ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dar es Salaam.
Vyama vya CCM na CUF ambavyo vimeunda serikali ya umoja wa kitaifa na kuwa na uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi na Bunge, wanategemewa kuwa wabunge katika Bunge la Katiba, hata hivyo misimamo yao imeanza kusigana na wao kugawanyika, jambo linaloweza kuathiri upatikanaji wa asilimia 50 ya kura ya maoni inayotakiwa kuungwa mkono visiwani humu.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar) Vuai Ali Vuai alisema mfumo uliopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba haukuzingatia masilahi ya taifa na ni hatari kwa mustakabali wa usalama wa Muungano wenyewe.

Vuai alisema mfumo huo unakwenda kinyume cha misingi iliyoachwa na waasisi wa muungano, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na mzee Abeid Aman Karume na kutaja kuwa visiwa vya Unguja na Pemba navyo havitabaki salama kama ilivyo sasa.

“Nitakuwa wa mwisho kukubali serikali tatu, siamini kabisa kama ni mfumo bora na imara, naota taifa likigawanyika na kukatika, najua na ninaamini kuwa Pemba na Unguja hazitakaa tena pamoja kama zilivyo sasa, hili tulitarajie,” alisema Vuai.

Aidha, alitaja mapendekezo ya rasimu hiyo kuwa licha ya kwenda kinyume cha sera ya Chama Cha Mapinduzi lakini pia ni kinyume cha sheria ya mabadiliko ya Katiba na kukiuka misingi ya kuanzishwa kwa taifa la Tanzania na mkataba wa Muungano.

Alisema Tume ya Warioba imejipa kazi na kujibebesha jukumu ambalo anaamini haikupewa kwa mujibu wa sheria na hadidu za rejea za tume hiyo na kutaka kuunda taifa jipya ndani ya taifa lililopo lililoishi kwa amani, utulivu na umoja.

“Chama Cha Mapinmduzi kitahakikisha wawakilishi na wabunge wake wanaendelea kutetea sera ya chama chao, sera yetu si kuwa na serikali tatu au nne, hatuwezi kubadilishiwa sera yetu na Warioba, tuna vikao halali vya kikatiba vya kubadili aidha sera, programu au miongozo yetu,” alisema Vuai.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, alisema mapendekezo yaliyomo katika rasimu ya pili ya Katiba yatasaidia kuendelea kudumisha Muungano na kuondoa kero za muda mrefu.

Bimani alisema kwa miaka takriban 50 serikali zote mbili zimekuwa zikiunda tume mbalimbali za kutatua kero na utekelezaji wake kushindikana hivyo mapendekezo ya Jaji Warioba yanahitaji kuungwa mkono na si kubezwa.

Aliwataka wabunge wa Bunge la Katiba kuweka pembeni mitazamo ya vyama vyao na badala yake watambue na kuthamini Zanzibar yao na utaifa na wasikubali kuburuzwa katika kutetea masilahi ya wananchi.

“Hii ni nafasi adimu na adhimu kwa taifa letu, Zanzibar yetu na masilahi ya kila upande, tuweke kando itikadi zetu za kisiasa, wabunge wafanye kazi moja muhimu ya kutetea wananchi na maendeleo yao,” alisema Bimani.

Hata hivyo aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Abdulrazaq Mussa Simai (Kwacha), aliwaambia waandishi wa habari kuwa viongozi wa SMZ na SMT lazima watafakari faida na hasara za kuvunjika kwa muungano.

Kwacha alisema rasimu hiyo ikipita uongozi wa CCM Bara na Zanzibar utalazimika kuwajibika kwa kushindwa kutetea sera yao ya msingi na ilani yake ambayo iliahidi kujenga muungano wa serikali mbili na si tatu.

Tokea kutangazwa kwa sera hiyo wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakijikusanya kwenye makundi na kujadili suala hilo ambalo linaonekana kuwakanganya huku baadhi ya watu wakitaka Zanzibar ipewe mamlaka kamili na wengine wakitaka ubaki mfumo wa serikali mbili.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company