Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zimetufikia, zinaeleza kwamba watuhumiwa ni jeshi la Polisi, na kwamba walirusha kitu kinachosadikiwa kuwa bomu - lililojeruhi 6, ambapo 4 kati yao wameruhusiwa baada ya matibabu kwenye hospitali ya Mission na ya Wilaya ya Arumeru.
Majira ya saa sita na nusu, waumini walidai kuona gari la polisi likipita kwa kasi, na lilipowakaribia walistuka mlipuko ukiwarusha pembeni, ambapo walijikuta na majeraha na usoni, mapajani na maeneo mbalimbali ya mwili. Kisha baada ya hapo gari ilisogea mbele na kuanza kurusha mabomu kwa watu wowote iliokutana nao.
Hadi sasa inaelezwa kuwa uchunguzi umeshaanza kufanyika, huku Kamanda Liberatus Sabas akikataa kuzungumzia zaidi suala hilo. Alipotafutwa na WAPO Radio FM, hakueleza kwa kina, lakini akasema kuwa sio suala la kwaya kama ambavyo imeelezwa, bali ni wakinadada wawili na kwamba hawezi kuzungumza zaidi, bali kesho (Ijumaa) atatoa taarifa rasmi na iliyo kamili kwa vyombo vya habari.
Alipoulizwa kuwa kama ni kweli jeshi la Polisi linatuhumiwa kuhusika, alisema kuwa atazungumza kesho kuhusiana na tukio hilo. Tukio hili limetokea ikiwa ni siku mbili zimepita tokea kuapishwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi mpya, Ernest Mangu ambaye amechukua nafasi ya IJP Said Mwema aliyestaafu.
Polisi wa idara mbalimbali wakiwa eneo la tukio kwenye tukio la mlipuko wa bomu jijini Arusha mnamo mwezi Mei 2013.
Mnamo mwezi Mei kulitokea mlipuko wa bomu kwenye kanisa katoliki Mtakatifu Joseph Olasiti ambapo lilihudhuriwa na Balozi wa Papa nchini, Francisca Padella.