MWILI wa Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa (63) aliyefariki dunia juzi nchini Afrika Kusini baada ya kuugua kwa muda mrefu unatarajiwa kuwasili nchini kesho.
Akitangaza ratiba ya kuwasili kwa mwili na maziko ya Waziri Mgimwa kwa waandishi wa habari jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema shughuli zote zitafanywa na serikali.
Lukuvi alisema tayari serikali imeshaunda kamati mbili, moja ipo jijini Dar es Salaam, ina wajumbe kutoka Ikulu, Wizara ya Fedha na Uchumi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo itaongozwa na yeye.
Alisema kamati ya pili imeundwa mkoani Iringa ambayo itashughulikia namna ya kuuhifadhi mwili wa marehemu Mgimwa kijijini kwake Magunga, ambayo itaongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Christine Ishengoma.
Lukuvi alisema mwili wa Mgimwa utawasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini, majira ya saa saba mchana katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal II) na kupelekwa nyumbani kwake Mikocheni B, na itakapofika majira ya saa 11 jioni utapelekwa katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo alisema siku ya Jumapili, mwili wa Mgimwa utawasili nyumbani kwake majira ya saa 5:30, kisha utapelekwa katika Ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya ibada, heshima za mwisho na salamu za rambirambi hadi saa nane mchana.
Alisema mara baada ya tukio hilo, mwili wa Mgimwa utapelekwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Teminal I) kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Iringa ambapo unatarajiwa kufika majira ya saa 10 jioni ili kuwapa fursa wananchi wa mkoa huo kuuaga katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Lukuvi alisema mara baada ya wananchi wa Iringa mjini kuaga, jioni hiyo hiyo mwili wa Mgimwa utapelekwa kijijini kwake Magunga kwa ajili ya kupumzishwa kesho yake (Jumatatu).
“Shughuli za kuwasili na hatimaye maziko zinafanywa na serikali kupitia kamati kuu na ile ya Mkoa wa Iringa, ambayo itapata mwongozo kutoka huko chini ya Dk. Ishengoma,” alisisitiza Lukuvi.
Akizungumza kwa masikitiko namna alivyomfahamu marehemu Mgimwa, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Salum, alisema amejifunza mengi kuhusu uongozi mara baada ya kuanza kufanya naye kazi walipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Mei mwaka jana.
“Kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu niliofanya kazi na Dk. Mgimwa, nimejifunza mengi katika uongozi. Kwani kazi kwake lilikuwa jambo la kwanza, kwa maana wakati mwingine alikuwa akikaa ofisini hadi saa 5 usiku, si hivyo tu bali hata siku za Jumamosi na Jumapili alikuwa akifanya kazi,” alisema.
Saada alisema alichojifunza kwake zaidi ni kwamba kama mtu anapewa dhamana ya uongozi anapaswa kuitimiza bila kuchoka na kulalamika.
Naibu waziri huyo ambaye hakutaka kusema ugonjwa uliosababisha mauti yake, alisema mara ya mwisho aliwasiliana na marehemu Mgimwa kwa simu mwezi mmoja uliopita na katika mazungumzo yao alimweleza kuwa anaendelea vizuri.
Katika hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini na Mkoa wa Iringa, kimesema kimepata pigo kwa kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, William Mgimwa.
Wakati serikali ya Mkoa wa Iringa ikiendelea na maandalizi ya mazishi ya Waziri Mgimwa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesitisha likizo yake iliyoanza hivi karibuni kutokana na msiba huo mkubwa kwa Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa nyakati tofauti mjini hapa, viongozi wa CCM wa wilaya na mkoa pamoja na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Gerald Guninita, walisema kifo cha Waziri Mgimwa si pigo tu kwa familia yake bali pia kwa taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, alisema kuwa CCM mkoani hapa imepata pigo kubwa kwa kumpoteza mbunge huyo na waziri na kuwa katika uhai wake Mgimwa alikuwa mbunge wa tofauti na wengine na kuwa siku zote hakuwa mbunge wa kujisikia kwa nafasi yake.
Kwani alisema mbali ya kuwatumikia vema wakazi wa Jimbo la Kalenga na Watanzania katika nafasi yake ya uwaziri wa Fedha na Uchumi, bado Mgimwa alikuwa kiongozi wa kushirikiana vema na chama na wananchi wake.
Alisema Mkoa wa Iringa umepata pigo kubwa juu ya kifo hicho na kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuenzi mchango wake katika kuyafanya yale yote ambayo katika uhai wake alikuwa akiyapigania na siku zote katika ndoto zake za kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kalenga.
“Tunaamini kila mtu ambaye amepata kufanya kazi na Dk. Mgimwa anatambua wazi kuwa alikuwa ni mchapa kazi na kiongozi mpenda watu…Dk. Mgimwa mbali ya kuwa waziri hakuwa na majivuno na alikuwa ni kiongozi wa misaada hata katika majukumu yasiyo rasmi katika nafasi yake…kweli sina cha kusema zaidi ya kuendelea na maandalizi ya mazishi yake,” alisema Msambatavangu.
Delophina Mwimbile Mtafilalo ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Iringa Vijijini, alisema bado viongozi wa CCM wa wilaya hiyo hawaamini kama Waziri Mgimwa amefariki dunia kwani tangu alipolazwa hawakupata nafasi ya kumjulia hali.
“Kweli tumepata pigo sana kwa kifo chake hadi sasa umetukuta tumesimama hapa nje tusijue la kufanya na hatujui sisi kama viongozi wa Jimbo la Kalenga ni nani ataziba pengo lake la ubunge,” alisema Delophina.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Gerald Guninita, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo alisema kifo cha Mgimwa kimepokewa kwa majonzi makubwa.
Mgimwa alifariki dunia juzi nchini Afrika Kusini alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago