Obama amwalika JK

RAIS wa Marekani, Barack Obama, amemwalika Rais Jakaya Kikwete kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika utakaofanyika jijini Washington baadaye mwaka huu.

Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Rajiv Shah, aliwasilisha mwaliko huo wakati wa mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) huko Davos, Uswisi.
Shah alisema Rais Obama amemwalika kuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika watakaohudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika utakaofanyika Agosti 5 hadi 6, jijini Washington.

Katika mwaliko huo, Rais Kikwete ameombwa kuchangia mawazo kuhusu jinsi gani ya kufanikisha mkutano huo utakaozungumzia jinsi Marekani inavyoweza kuongeza kasi ya kusambaza umeme barani Afrika chini ya mpango wa Marekani wa Power Africa.

Hata hivyo, Rais Kikwete aliukubali mwaliko huo na kusema atawasilisha mapendekezo yake ili kufanikisha mkutano huo. Hii ni mara ya tatu kwa Rais Obama kumwalika Rais Kikwete kushiriki katika shughuli zake.

Miezi mitatu baada ya kushika madaraka mwaka 2008, Obama alimwalika Kikwete kuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kutembelea Ikulu na kufanya mazungumzo naye.

Wakati huohuo, Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amemwalika Rais Kikwete kuhudhuria mkutano wa Taasisi ya Uchumi Duniani Afrika (WEF-Africa) utakaofanyika jijini Abuja, Nigeria Mei 7 hadi 9.

Rais Jonathan alitoa mwaliko huo walipokutana na kufanya mazungumzo jana jijini Davos, Uswisi ambako viongozi hao wanahudhuria mkutano wa WEF, ombi ambalo Rais Kikwete alilikubali.

Nigeria inakuwa nchi ya nne barani Afrika kuandaa mkutano huo.

Kwa miaka mingi, mkutano wa WEF-Africa ulikuwa unafanyika Cape Town, Afrika Kusini hadi Tanzania ilipofanikiwa kuwa ya kwanza baada ya nchi hiyo kuwa mwenyeji wa mkutano huo mwaka 2010.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company