Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Ulaya wamenza kusimamia usalama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bangui huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, ikiwa ni operesheni yao kubwa ya kwanza ya kujaribu kuhitimisha mauaji dhidi ya Waislamu yanayoendelea nchini humo kwa miezi kadhaa sasa.
Kabla ya hapo uwanja wa ndege wa Bangui ulikuwa ukisimamiwa na askari wa Ufaransa, na katika sehemu hiyo kuna maelfu ya wakimbizi wanaopata hifadhi baada ya kukimbia machafuko yanayowalenga Waislamu. Taarifa zinaeleza kuwa kundi la Kikristo la Anti Balaka linawashambulia Waislamu katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja na kuchoma nyumba zao na kuharibu mali na misikiti yao.
Kuna askari 2,000 wa Ufaransa na 5,000 wa Kiafrika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini hadi sasa wameshindwa kurejesha amani na usalama kwenye nchi hiyo.