Sudan: Uganda inawaunga mkono waasi Blue Nile

CHANZO REDIO TEHARAN KISWAHILI
Serikali ya Sudan kwa mara nyingine tena imeituhumu Uganda kuwa inawaunga mkono waasi wa nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Sudan imesisitiza kuwa, Uganda inapasa kuacha mara moja uungaji mkono wake kwa makundi ya waasi yanayopigana na serikali ya Khartoum. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Sudan imeongeza kuwa, serikali ya Uganda inawapatia hifadhi viongozi wa makundi ya waasi sanjari na kuandaa vikao vya viongozi hao mjini Kampala kwa shabaha ya kupanga mikakati ya kuisambaratisha serikali ya Rais Omar Hassan al Bashir. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, serikali ya Sudan iliwahi kuwasilisha mashtaka yake dhidi ya Uganda mwaka 2013 kwenye kikao cha 12 cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Cairo Misri, na pia kwenye kikao cha kimataifa cha Ukanda wa Maziwa Makubwa ya Afrika (ICGLR) kilichofanyika mwaka 2011. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha ICGLR ni kwamba, ni marufuku kwa mwanachama wa ukanda huo kuyaunga mkono makundi ya waasi yanayopigana na nchi nyingine mwanachama. Makundi ya waasi nchini Sudan yamejizatiti zaidi katika majimbo ya Blue Nile lililoko kusini mwa Sudan na Kordofan Kusini lililoko katika eneo la Darfur, magharibi mwa nchi hiyo.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company