Uchaguzi kufanyika Iraq
Wapiga kura nchini Iraq wanashiriki katika zoezi la upigaji kura katika mikoa yote isipokuwa mkoa mmoja katika uchaguzi wa kwanza wa wabunge tangu wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo mwaka 2011.
Waziri mkuu wa sasa Nouri al-Maliki anagombea kiti chake kwa muhula wa tatu lakini kampeni zimekuwa zikipigwa kwa misingi ya vurugu za kisiasa zinazoendelea kukithiri nchini humo.
Selikali ya muungano ya bwana Maliki inayoongozwa na chama cha Kishia imekabiliwa na wakati mgumu kupambana na uasi unaongozwa na kundi lenye ufungamano na Al Qaeda katika mji wa Falluja na mkoa wa Anbar.
Sauti za mizinga zimekua taswira ya kila siku katika baadhi ya maeneo ya Iraq wakati kampeni za kuelekea uchaguzi huu.
Matokeo yake ni mashambulio ya kujitolea mhanga karibu kila siku.
Uchaguzi kufanyika Iraq
Helikopta za kijeshi zinashika doria katika anga ya Baghdad na serikali imefunga uwanja wa ndege na baadhi ya barabara kuu ndani na nje ya mji huo.
Hatua hizo zinanuia kuwapa imani wapigaji kura watakaojitokeza kwani ni bayana kuwa huenda vituo vya kupigia kura vikalengwa.
Watu 160 wameuawa wiki iliyopita huku wengine 275 wakijeruhiwa.
Baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa vikosi vya usalama vimepoteza maafisa elfu moja mwaka huu kwenye mapigano ya kukabiliana na uasi katika maeneo ya Fallujah na Anbar.
Inatabiriwa kuwa huenda Bw Maliki akashinda awamu ya tatu na kumuwezesha kuunda serikali ya muungano lakini ni bayana kuwa swala la usalama litasalia kuwa changamoto kubwa.