Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
BONDIA Francis Miyeyusho kesho kwenye ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam atajaribu kurejesha heshima wakati atakapopigana na Mohamed Matumla katika pambano lisilo la ubingwa, uzito wa Feather baada ya Aprili 19, mwaka huu kupigwa vibaya na Sukkassem Kietyongyuth wa Thailand.
Lakini kuna wasiwasi pambano la kesho likawa chungu tena Miyeyusho ‘Chichi Mawe’, kwani ni takriban wiki tatu tangu apigwe Mthailand na hakuna hakika kama alipata muda mzuri wa kupumzika na kujiandaa na pambano lingine.
Nitakuua kesho; Mabondia Mohamed Matumla kulia na Francis Miyeyusho kushoto wakitunishiana misuli leo wakati wa kupima uzito.
Ikumbukwe Miyeyusho alipigwa na Sukkassem kwa Knockout (KO) raundi ya kwanza sekunde ya 55 katika pambano la raundi 10 lisilo la ubingwa, uzito wa Feather lililofanyika ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam.
Katika pambano hilo lililohudhuriwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyekuwa mgeni rasmi, Miyeyusho aligoma kupanda ulingoni kwa dakika zaidi ya 20 akishinikiza kwanza alipwe fedha zake.
Kamanda Kova ambaye mdogo wake, Mussa Kova ndiye aliyeandaa mapambano hayo kupitia kampuni yake ya Mawenzi Production, aliingilia sakata hilo na bondia huyo akalipwa fedha zake akapanda ulingoni.
Dalili za Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ kupigwa zilionekana wakati nyimbo za taifa zinapigwa, kwani alikuwa asiyejiamini na mwenye kihoro, hivyo kumpa nafasi Mthailand kulianza kwa kasi pambano hilo.
Miyeyusho akiwa chini baada ya kudondoshwa na Mthailand na chini ni refa Emmanuel Mlundwa akiwaamulia kumuokoa Mtanzania huyo aliyekuwa akiadhibiwa bila majibu na mpinzani wake
Mgeni alianza kumtandika Miyeyusho tangu sekunde ya kwanza na ndani ya sekunde 20 bondia wa nyumbani alikaa chini akawahi kusimama, hata hivyo pigo hilo lilimuondoa mchezoni kabisa Chichi.
Mthailand aliibaini hali hiyo na akamfuata kwenye kamba Miyeyusho kumsukumia makonde mfululizo hadi refa Emmanuel Mlundwa alipokwenda kusimamisha pambano.
Refa alimpa nafasi Miyeyusho kuamua kuendelea au la na bondia huyo akajaribu kusogea mbele kurudi mchezoni, lakini akadondoka na Mlundwa akamaliza pambano, huku Chichi akisaidiwa na wasaidizi wake kuinuliwa chini kutolewa ulingoni.
Sasa kesho tena, katika ukumbi ule ule- Miyeyusho anakwenda kukutana na bondia mwingine mzuri anayechipukia nchini, mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia uzito wa Light Middle, Rashid Matumla.
Ikumbukwe Matumla mdogo atataka kumlipia kisasi baba yake mdogo, Mbwana Matumla ambaye alistaafishwa ngumi na Miyeyusho kwa kipigo kikali Oktoba 30, mwaka 2011.
Pambano la kesho litakuwa la 51 kwa Miyeyusho tangu aanze kupigana kifua wazi Februari 1, mwaka 1998 akiwa ameshinda mapambano 37, kati ya hayo 23 kwa KO na kupigwa 11, kati ya hayo 10 kwa KO na sare mawili.
Mtoto wa Rashid Matumla ambaye ngumi katika ukoo wao zinaanzia kwa babu yake Mzee Ally Matumla, kwake hilo litakuwa pambano la 15 tangu ajitose kwenye ngumi za kulipwa Novemba 17, mwaka 2010 akiwa ameshinda mapambano 11, manne kwa KO na ametoka sare mara tatu akiwa hajapoteza pambano hadi sasa.
Pambano la kesho linatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa wa kishabiki, baina ya wakazi wa Keko na Temeke kwa ujumla watakaokwenda kumsapoti Matumla na wakazi wa Manzese na Kinondoni kwa ujumla watakaokwenda kumsapoti Miyeyusho. Je, ni Miyeyusho atarejesha heshima, au Matumla atamilipia kisasi baba kesho? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago