NA AUGUSTA NJOJI
Samuel Sitta
Maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kukakataa uwezekano wowote wa kufanyika kwa mazungumzo ama baina yake au kiongozi yeyote wa serikali na Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa), umevunja juhudi za Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, kutaka kukutana na umoja huo kwa mazungumzo.
Chama hicho kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, jana kilitangaza rasmi mjini hapa kwamba hakina mpango wa kuzungumza au kuishawishi serikali au viongozi wake kutafuta ufumbuzi ili Ukawa warejee bungeni.
Nape alitoa msimamo baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kilichofanyika juzi chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Alisema hakuna sababu ya kuendelea kuwabembeleza Ukawa na kwamba watapingana nao na kuwashughulikia huko huko kwa wananchi wanapokwenda.
Baada ya Ukawa unaoundwa na wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Chadema, Cuf na NCCR-Mageuzi, kutoka bungeni Aprili 16, mwaka huu wakituhumu wajumbe wa CCM kwa ubaguzi, kejeli na uchakachuaji wa Rasimu ya Katiba, Aprili 21, mwaka huu Sitta alianza juhudi za kukutana nao nje ya Bunge, lakini hakufanikiwa licha ya kukutana na Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Sitta alikutana na Maalim Seif Zanzibar baada ya kukutana pia na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Muhamed Shein na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume. Wote alikutana nao Zanzibar.
Akijibu ombi la mbunge wa Bunge Maalum la Katiba, Hamsi Kambaya, aliyemsihi Sitta kukutana na Ukawa, alisema kuwa kazi hiyo imekwisha kuanza, akirejea safari yake ya Zanzibar na mazungumzo na viongozi hao.
Jana Nape pia alisema CC iliitaka Sekretarieti na wanachama na wote wanaoitakia nchi mema kuendelea kujibu kila uongo unaozungumzwa na ujibiwe kwa uzito unaostahili.
“Mimi nakwambia kutokuwapo kwao bungeni kumetulia sana naona waendelee kukaa mtaani na wanaotaka Katiba itungwe waendelee na kazi … watu wenyewe hawajai mkononi, hiyo theluthi mbili inapatikana bila wao kwa nini tuwabembeleze,” alijigamba Nape bila kufafanua theluthi hiyo itapatikana kwa wajumbe wa bara au na Visiwani kama sheria inavyotaka.
Aidha, Nape alisema CC imesikitishwa na kitendo cha wajumbe wa Ukawa kususia Bunge hilo na kuamua kwenda kwa wananchi.
“CCM inapenda kuwakumbusha kuwa muda wa kupeleka rasimu kwa wananchi bado, muda huo utafika mchakato wa Bunge Maalum la Katiba utakapokuwa umemalizika kwa mujibu wa sheria,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa kwa sasa bado sheria inawataka ukamilishwe kwanza mchakato wa Bunge Maalum la Katiba ndipo waende kwa wananchi.
Pia, Nape alisema CC inasikitishwa na juhudi za makusudi za baadhi ya watu au vikundi kuamua kuendeleza upotoshaji wa makusudi kupotosha mchakato mzima wa Bunge Maalum la Katiba.
“Kuna baadhi ya watu au vikundi kwa makusudi kabisa wameamua kupotosha mchakato huu kwa kwenda barabarani kufanya mikutano … CCM itaendelea kujibu kila uongo unaoenezwa, tayari tumefanya mikutano mikubwa Pemba na Unguja yenye mafanikio na tumewafunika,” alisema.
Nape alisema CC imepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Sekretarieti ya chama na watendaji kwa ujumla wa CCM kwa kuamua kujibu kila uongo na uchochezi unaofanywa wa watu wasioutakia mema mchakato wa Katiba.
“Lengo ni kuendelea kulinda maslahi ya nchi, umoja na mshikamano kila anayeeneza maneno ya uongo atajibiwa kwa wakati na kwa uzito unaostahili,” alisema na kuongeza:
“Kama wao wanaeneza uongo basi CCM kitaeneza ukweli, tutawaambia Watanzania ukweli, lengo ni kulinda maslahi ya nchi, umoja na mshikamano wa nchi yetu, hatutakaa kimya.”
Hata hivyo, alisema chama hicho kinawahakikishia wananchi na Watanzania wote wanaoitakia mema nchi kuwa kina nia thabiti ya kuhakikisha inapatikana katiba mpya.
Alisema CC imeridhishwa na tathmini iliyofanywa pamoja na mapungufu yaliyojitokeza na jinsi mchakato mzima unavyoendelea.
“Wamekikimbia chombo cha sheria badala yake wamekimbilia wananchi…CC inawapongeza wazalendo waliobaki ndani ya Bunge
Maalum na kuendelea kubaki ndani kwa ajili ya mchakato wa kuandika Katiba mpya,” alisema Nape.
Hadi Bunge linahairishwa Aprili 25, mwaka huu, wajumbe hao walikuwa nje ya Bunge na hadi sasa wameapa kwamba hawatarejea na wataendelea kufanya mikutano ya kuwaeleza wananchi kuhusu kilichotokea katiba bunge hilo.
WARIOBA: NITAENDELEA KUHESHIMU MAONI YA WANANCHI
Wakati huo huo, Jaji Warioba amesema pamoja na yeye kuwa mwanachama wa CCM, lakini ataendelea kuamini maoni yaliyotolewa na wananchi yaliyomo katika rasimu ya katiba.
Jaji Warioba alisema hayo juzi usiku wakati akizungumza katika sehemu ya pili ya mahojiano yake na kituo cha televisheni cha ITV katika kipindi cha dakika 45.
Alisema tume ilikuwa na wajumbe zaidi ya 30 kutoka makundi mbalimbali na vyama vya siasa, lakini waliweka misimamo ya vyama vyao pembeni na kufanya kazi ya taifa kwa kusikiliza wanachokisema wananchi.
Alisema alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo hakuamini kama angeliweza kuunganisha timu iliyoteuliwa kukusanya maoni ya katiba kwa kuwa kila mmoja alikuwa ametoka katika chama au kundi lake.
“Wakati nateuliwa kuwa mwenyekiti wa tume kulikuwa na watu kutoka sehemu mbalimbali kwa hiyo tulikubaliana kwamba hata kama umetoka CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na makundi mengine inatubidi tuondoe misimamo ya vyama vyetu, ili tuweze kufikia malengo ya Watanzania,” alisema na kuongeza:
“Kama nilivyosema, nilipotoa taarifa mwanzoni kabisa nilipoteuliwa baada ya kuona kundi nilikuwa nalo sikuamini kama tutatoka na kundi litakounganisha Watanzania. Kwa kuwa sisi kama Watanzania tuliona tumepewa kazi na taifa, tutakuwa waaminifu na tutakwenda kuwasikiliza Watanzania tupendekeze kama wanavyotaka wao na si vinginevyo.”
Aidha, Jaji Warioba alisema anashangazwa na kauli ya mjumbe mmoja wa Bunge Maalum la Katiba kutoka katika Kamati Namba Moja aliyesimama katika bunge hilo na kutoa taarifa kwamba tume hiyo haikutumwa kufanya kazi ya kuuliza muundo wa Muungano.
“Kwanza namshangaa yule mama aliyetoa taarifa ya Kamati Namba Moja akisema kwamba hatukuwatuma Tume ya Katiba kwenda kufanya kazi hii. Sisi tumefanya kazi kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia sheria,” alisema Jaji Warioba.
“Popote tulipokuwa tunapita, jambo ambalo tulizingatia ni uwapo wa Muungano, na sheria haikusema tuzingatie muundo wa serikali mbili bali uwapo wa Muungano. Na wananchi ndio walizungumzia muundo wa Muungano, kwa hiyo tukaangalia hoja zilizopo na uhalisia wa utulivu,” alisema.
Alisema wananchi wengi walipendekeza serikali tatu kwa hoja, na kueleza bayana matatizo ambayo ikiwa yatatokea ikiwa muundo wa serikali mbili utaendelea.
Kuhusu baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kumtukana na kumbeza, Jaji Warioba alisema haoni kama ni tatizo na kwamba wanachojivunia wajumbe wa Tume hiyo ni kwamba walipewa dhamana ya kuitafutia Tanzania Katiba mpya ambayo ni matarajio ya wengi.
Aliwashauri wajumbe wa bunge hilo kukaa pamoja na kuondoa tofauti zao za kivyama ili Watanzania wapate Katiba mpya yenye maslahi ya taifa.
Pia, alivishauri vyama vya siasa kuacha kuangalia maslahi yake badala yake viangalie maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
CHANZO: NIPASHE
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago