Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Eng. Gerson Lwenge akifafanua jambo wakati wa kikao cha Kamati ya Miundombinu kujadili bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2014/15.
Baadhi ya Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Wizara ya Ujenzi wakiwa katika kikao cha kujadili bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2014/15.
KAMATI YA BUNGE YAPITISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI
Kamati ya Miundombinu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapema wiki hii ilikutana na Watendaji wa Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya kupitia maepndekezo ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2014/15.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli awali kabla ya kuwasilisha mapendekezo hayo kwanza alianza kwa kutoa tarifa ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 ambapo Wizara ya Ujenzi ilitengewa Shilingi 381,205,760,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Hadi kufikia mwezi Aprili 2014 jumla ya Shilingi 372,088,829,186.73 zilikuwa tayari zimetolewa na HAZINA. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 97.61 ya kiasi kilichokuwa kimepangwa.
Akizungumzia fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund), Waziri wa Ujenzi alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 Mfuko huo ulipangiwa kukusanya Shilingi 504,306,000,000 kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi, TANROADS na TAMISEMI. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2014 fedha zote zilizokusanywa zilikuwa zimefikia Shilingi bilioni 496.220 sawa na asilimia 98.4 ya malengo ya mwaka huu wa 2013/14.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. Magufuli akiwasilisha mapendekezo ya bajeti kwa mwaka ujao wa 2014/15 alifafanua kuwa ili Wizara ya Ujenzi ili iweze kutekeleza majukumu na malengo yake itahitaji kiasi cha Shilingi trilioni moja, bilioni mia mbili kumi na tisa, milioni mia saba kumi na saba, mia tano tisini na mbili elfu (1,219,717,592,000.00). Fedha hizo zimeelezewa kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na miradi ya maendeleo.
Kamati hiyo ya Bunge baada ya kupitia vipengele vyote ilihitimisha kikao hicho kwa kupitisha mapendekezo hayo ya Wizara ya Ujenzi ili yaweze kuwasilishwa rasmi katika Mkutano unaoendelea wa Bunge la Bajeti.
Hata hivyo katika hatua nyingine, Kamati hiyo iliitaka Wizara hiyo ya Ujenzi kuhakikisha inasimamia ipasavyo sheria na taratibi zilizowekwa kwa lengo la kulinda miundombinu mbali mbali inayosimamiwa na wizara hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Serukamba alisisitiza kuwa kuwepo kwa matuta barabarani pamoja na kutosimamia ipasavyo udhibiti wa uzito wa magari hasa makubwa katika barabara zetu huathiri kwa kiasi kikubwa miundombinu hiyo.