Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewasihi viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea katika vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyotarajiwa kuendelea tena kuanzia Agosti 5 mwaka huu.
Amesema kama tatizo la wajumbe wa umoja huo kususia vikao vya Bunge hilo wiki moja kabla ya kuahirishwa kwake ni kejeli na matusi kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, jambo hilo linazungumzika.
Waziri Pinda alitoa kauli hiyo jana wakati wa kuhitimisha na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2014/15.
Mei 7 mwaka huu, Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati akitoa hotuba yake kuhusu Bajeti ya Waziri Mkuu, alisema wajumbe wa Ukawa hawatarejea katika Bunge la Katiba mpaka watakapohakikisha kuwa maana halisi ya uwepo wa Bunge hilo unafuatwa.
Alisema kama lengo ni kutumia mwamvuli wa Bunge Maalumu la Katiba ili kuendeleza mfumo wa kikatiba na muundo wa muungano uliopo sasa, wajumbe wa Ukawa hawatakuwa sehemu ya usaliti huo kwa Watanzania, huku akisisitiza kukerwa kwake na lugha za matusi na kejeli dhidi yao zilizokuwa zikitolewa na wajumbe kutoka chama tawala.
Hata hivyo Pinda jana alisema “Kauli zilizotolewa na Mbowe zilikuwa kali na zilinitisha kidogo. Nadhani tusianze kutoa picha kwa Watanzania juu ya hali ya kutokuwepo kwa amani katika siku zijazo kwa sababu jambo hili siyo zuri,” alisema Pinda na kuongeza;
“Nadhani kubwa hapa ni kuendelea kuzungumza juu ya uwezekano wa namna ya kufikia hatima nzuri juu ya mchakato wa Katiba.”
Pinda alisema sababu za lugha za kejeli na matusi zilizotolewa na Mbowe siyo sababu ya msingi ya kuwafanya wajumbe wa Ukawa kususia vikao vya Bunge hilo.
“Hata kama tungefikia mahali tukavutana sana, suluhu haikuwa kutoka nje ya Bunge. Hata kama mngesema liahirishwe ili tukajadiliane na kukubaliana na kisha kurejea na kuendelea na mjadala, sidhani kama lingekuwa tatizo.”
Waziri Pinda alisema Rais Jakaya Kikwete hakuwa chanzo cha kuvuruga mchakato wa Katiba kama ilivyoelezwa na Mbowe na kufafanua kuwa Rais Kikwete kama wananchi wengine naye alikuwa akitoa maoni yake na kwamba alieleza wazi kuwa wabunge ndiyo wenye uamuzi wa mwisho.
Huku akiwataja wajumbe kadhaa wa Ukawa, Pinda alisema: “Bado naamini Mbowe, James Mbatia, John Cheyo na Profesa Ibrahim Lipumba tunaweza kuzungumza, maana kama hoja ni matusi na kejeli, hivi tukikubaliana si tunarudi na kukubaliana kutokuwapo kwa vitu hivyo.”
Alisema kuwa anaunga mkono kauli ya Mbowe ya kukutanisha makundi yote yanayopingana ili kuzungumza ili yaweze kukubaliana.