Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa nchi yake na Pakistan unapaswa kujengeka juu ya misingi ya kuimarisha usalama na ustawi katika mipaka ya nchi mbili. Dk Hassan Rouhani amesema hayo leo wakati alipoonana na Waziri Mkuu wa Pakistan Bw. Muhammad Nawaz Sharif, hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, mipaka ya nchi hizi mbili ni mirefu na ni muhimu. Ameongeza kuwa: Iran iko tayari kuyaunganisha maeneo ya mipaka ya nchi hizi mbili kwa njia za reli, barabara na mkongo wa mawasiliano. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ametaka kuimarisha ushirikiano wa kiutamaduni na kiuchumi na Pakistan hususan katika mikoa ya Iran inayopakana na nchi hiyo na kuelezea matumaini yake kuwa, kupanuliwa kanali ya kupeleka umeme wa Iran nchini Pakistan kutastawisha ushirikiano wa kiuchumi wa nchi mbili. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Pakistan, Muhammad Nawaz Sharif amesema kuwa, uhusiano wa kihistoria na kidini baina ya nchi yake na Iran ni mkubwa sana na ameelezea matumaini yake kuwa safari za viongozi wa Pakistan mjini Tehran zitafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya nchi hizi ndugu. Pia amesema nchi yake iko tayari kuondoa vizuizi vyote vinavyokwamisha ufanikishaji wa mradi wa kupelekwa gesi ya Iran nchini Pakistan na kuongeza kuwa, ushirikiano wa nchi hizi mbili katika masuala ya kupambana na ugaidi ndio unaoweza kuleta amani ya kudumu katika mipaka ya nchi hizo.