Rais Jakaya mrisho Kikwete wa Tanzania, ametaka kuimarishwa usalama na amani katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Rais Kikwete ameyasema hayo mjini Kinshasa na kusisitiza kuwa, kuna haja ya kurejeshwa amani huko mashariki mwa Kongo baada ya kushuhudiwa machafuko ya muda mrefu ya waasi. Aidha Rais wa Tanzania ameashiria uhusiano mwema uliopo kati ya Dar es Salam na Kinshasa kwa kusema kuwa, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi mbili zenye ujirani mwema na hivyo akataka kuimarishwa zaidi uhusiano mwema katika uwanja wa uchumi. Tanzania ni moja ya nchi zenye askari wake nchini Kongo chini ya mwavuli wa askari wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani (MONUSCO). Licha ya kundi la M23 moja ya makundi makubwa yaliyokuwa yakiendesha vita dhidi ya serikali ya Kinshasa kuweka chini silaha na kujiunga na mwendneo wa amani nchini humo, lakini bado maeneo ya mashariki mwa taifa hilo la katikati mwa Afrika yanaendelea kushuhudia machafuko, kutokana na kuwepo wa makundi ya waasi kama vile Mai-Mai. Rwanda na Uganda ni nchi mbili jirani ambazo zimekuwa zikinyoshewa kidole cha lawama zikidaiwa kuwaunga mkono waasi dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.