SOMA; MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO), MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.) KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2014/2015


(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefikisha umri wa nusu karne tangu ilipozaliwa tarehe 26 Aprili, 1964. Kama anavyosema Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda katika hotuba yake ya tarehe 7 Mei, 2014 ‘Kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2014/2015’: “Miaka 50 kwa lugha yoyote ile siyo kipindi kifupi.” Waziri Mkuu ametumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinazoonyesha kwamba asilimia 90.6 ya Watanzania wote “wamezaliwa ndani ya Muungano na nchi wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Kwa maneno ya Waziri Mkuu, “sote tunawajibika kuwatendea haki watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu.”
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyo kwa Watanzania wengine wengi, na mimi pia nimezaliwa ndani ya Muungano. Ninaamini kwamba ukweli huu unawahusu pia waheshimiwa wabunge wengi waliomo ndani ya Bunge hili tukufu. Na sisi pia tunaomba kutendewa haki kuhusu Muungano huu. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, haki tunayoomba kutendewa ni moja tu: kuambiwa ukweli juu ya Muungano huu na historia yake, hali yake ya sasa na mwelekeo wake wa baadaye. Haki tunayoomba kutendewa ni kwa watawala kuacha propaganda na uongo juu ya Muungano na kutuambia ukweli wote juu ya Muungano huu.
Bob Marley, aliyekuwa mwanamuziki mpigania uhuru wa watu weusi maarufu kutoka Jamaica, aliwahi kusema katika wimbo wake ‘Get Up, Stand UP, Stand Up For Your Rights’ (‘Amkeni, Simameni, Simameni kwa Haki Zenu’) kwamba: “You can fool some people some time, but you cannot fool all the people all the time”, yaani, unaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa muda fulani, lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote! Baada ya nusu karne ya uongo na propaganda kuhusu Muungano huu, Watanzania wa kizazi hiki cha Muungano wanataka ukweli.
Na Watanzania hawa hawataulinda, wala kuuimarisha au kuudumisha Muungano huu endapo wataendelea kudanganywa au kufichwa ukweli juu ya mambo mengi yanayouhusu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, sisi kizazi cha Muungano tunahitaji kutendewa haki: acheni propaganda na uongo kuhusu Muungano huu ndipo muweze kutuambia tuulinde, tuuimarishe na tuudumishe!
SHEREHE ZA MUUNGANO NA ‘WAASISI’ WA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Sherehe za Miaka 50 ya Muungano ni mahali pazuri pa kuanzia kudai ukweli juu ya Muungano huu. Mtu yeyote anayetembea sasa katika Barabara ya Nyerere kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi katikati ya jiji la Dar es Salaam; au Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kuanzia Morocco hadi katikati ya jiji, ataona kila mlingoti wa taa za barabarani umepambwa kwa picha za Waasisi rasmi wa Muungano, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, wakiwa katika matukio mbali mbali ya siku za mwanzo za Muungano. Picha hizo za Waasisi hao pia zimepambwa karibu kila mahali katika barabara za katikati ya Eneo Kuu la Kibiashara (CBD) la Jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar, barabara zote kuu za Mji wa Zanzibar, ikiwamo ile inayotoka Mji Mkongwe kupitia Ikulu ya Zanzibar hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, hakuna picha hata moja ya Waasisi wa Muungano katika matukio yanayoonyeshwa kwenye picha zilizoko Dar es Salaam. Badala yake, barabara hizo zimepambwa kwa picha za Marais wa Zanzibar toka Mapinduzi ya mwaka 1964 hadi wa sasa. Ni ndani ya eneo la wageni maarufu (VIP) pekee ndio kuna picha moja ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume. Hii ni katika wiki ambayo Muungano huu umeadhimisha miaka hamsini tangu kuzaliwa kwake!
Kwa jinsi ambavyo tangu mwaka huu uanze Watanzania tumepigwa propaganda za kila aina juu ya Muungano na TBC na vyombo vingine vya habari vya serikali na vya binafsi, kukosekana kwa dalili yoyote ya sherehe za Muungano kwa upande wa Zanzibar wakati wa kilele cha sherehe hizo kunatilia shaka juu ya uimara wa misingi ya Muungano wenyewe. Hii ndio kusema kwamba pengine kuna ukweli katika hitimisho la Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba Tanganyika ndiyo imevaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na pengine ndio maana Muungano huu haujawahi kuungwa mkono Zanzibar kwa kiasi ambacho wanaopenda kutuaminisha vinginevyo wamekuwa wakidai. Aidha, pengine ndio maana hata picha za kuchanganya udongo zinazoonyeshwa na TBC kila kukicha zinamwonyesha Mwalimu Nyerere akichanganya udongo peke yake, wakati Sheikh Karume haonekani kabisa!
Mheshimiwa Spika,
Kuna jambo lingine linalofikirisha sana kuhusu picha hizi za Sherehe za Miaka Hamsini ya Muungano zilizopamba mitaa ya Dar es Salaam. Baadhi ya picha hizo zinawaonyesha watu wengine ambao wamefutwa kabisa katika historia rasmi wanayofundishwa watoto wetu mashuleni na vyuoni. Hivyo, kwa mfano, katika picha maarufu ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume wakisaini Hati za Makubaliano ya Muungano wapo pia, kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde, wakati kwa upande wa Zanzibar wanaoonekana kwenye picha hiyo ni Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo. Aidha, kuna picha inayowaonyesha Mwalimu Nyerere, Sheikh Karume na Kassim Hanga wakitabasamu kwa furaha kubwa.
Katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabiakilichochapishwa mwaka 2010, Harith Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo Oscar Kambona, Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida walitoa mchango mkubwa katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, na baadaye kufanikisha Muungano na Tanganyika wa Aprili 26 ya mwaka huo. Katika kitabu chake The Partner-ship: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Miaka 30 ya Dhoruba, Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe ameeleza kwamba ni Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde ndio waliompelekea Sheikh Karume nakala za Hati ya Makubaliano ya Muungano kabla ya Hati hizo kusainiwa tarehe 22 Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Swali kuu ambalo sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka lijibiwe kwa ukweli kabisa ni ‘waasisi’ hawa wengine wa Muungano, akina Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida kwa upande wa Zanzibar; na Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde kwa upande wa Tanganyika walipotelea wapi na kwanini hawatajwi katika historia rasmi ya Muungano na waasisi wake? Kassim Hanga alikuwa Waziri Mkuu na baadaye Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; wakati Twala alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo na Saleh Saadalla alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye wakati wa kuzaliwa kwa Muungano; Bhoke Munanka alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya masuala ya usalama, na Job Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.
Katika Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!, Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo akina Hanga, Twala na Saadalla pamoja na viongozi wengine waandamizi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama vile Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa waliuawa na kuzikwa katika handaki moja katika sehemu inayoitwa Kama, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja. Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo. Aidha, tunataka kuambiwa ukweli kwanini mchango wao katika kuzaliwa kwa Muungano umefichwa kwa muda wote wa nusu karne ya Muungano huu.
Kuhusu Oscar Kambona, inafahamika kwamba katika miaka ya mwisho ya ukoloni na miaka ya mwanzo ya uhuru, ‘mwasisi’ huyu wa Muungano alikuwa mtu wa karibu sana wa Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere ndiye alikuwa ‘Best Man’ wa Kambona wakati wa harusi yake iliyofanyika London, Uingereza mwaka 1960. Inafahamika, hata hivyo, kwamba mwaka 1967 Oscar Kambona alikosana na Mwalimu Nyerere na akalazimika kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza alikoishi hadi aliporudi nyumbani wakati wa kurudishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.
Tuliosoma miaka ya sabini na ya themanini tulifundishwa mashuleni na kuimbishwa nyimbo zilizotuaminisha kwamba Oscar Kambona alikuwa msaliti aliyetaka kuipindua Serikali yetu tukufu. Hata hivyo, hatukuwahi kuambiwa kama alishtakiwa katika mahakama yoyote ya hapa nchini na, kama ni hivyo, kama alipatikana na hatia yoyote na kuadhibiwa na mahakama. Tunachojua ni kwamba aliporudi nyumbani mwaka 1992, Mzee Kambona hakukamatwa wala kushtakiwa kwa kosa lolote lile. Sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano huu tunataka tutendewe haki kwa kuambiwa ukweli juu ya tuhuma za usaliti dhidi ya Mzee Oscar Kambona ambaye sasa anaandikiwa vitabu kuwa ni mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kuzaliwa kwa Muungano huu.





KUTOLEWA KWA NYARAKA ZA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Katika maoni yake wakati wa Bunge la Bajeti la mwaka wa fedha 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kwamba Serikali iweke wazi “nyaraka mbali mbali zinazohusu historia ya Muungano wetu na ‘mapito’ yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyotokea yanayouhusu. Hii ni muhimu zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba mataifa ya magharibi kama vile Marekani na Uingereza yalikwishatoa hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na balozi zao za Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa hayo zilihusika katika kuzaliwa kwa Muungano.”
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilifafanua kwamba “kuanikwa kwa nyaraka zilizoko katika mamlaka mbali mbali za Serikali kutasaidia kuthibitisha au kukanusha taarifa ambazo chanzo chake ni nyaraka za kidiplomasia na kijasusi za nchi hizo kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na njama za kibeberu za kudhibiti ushawishi wa siasa za kimapinduzi za Chama cha Umma na viongozi wake ndani ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar la wakati huo. Aidha, nyaraka hizo zitatoa mwanga juu ya kilichowasibu viongozi waandamizi wa chama hicho ambao bila uwepo wao kutambuliwa rasmi, historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano inabaki pungufu.”
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilisisitiza juu ya haja ya taifa letu kuambiwa ukweli juu ya Muungano huu: “... Miaka karibu hamsini ya Muungano ni umri wa kutosha kwa taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote juu ya kuzaliwa kwake na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho.” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirudia wito wake huo wakati wa kuwasilisha maoni yake juu ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka jana.
Mheshimiwa Spika,
Mjadala juu ya nyaraka za Muungano huu ulichukua picha mpya wakati wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba walipohoji uwepo wa Hati ya Makubaliano ya Muungano na uhalali wa Muungano wenyewe wakati wa mjadala juu ya Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba. Baada ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne kuonyesha ushahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijawahi kuwa na nakala ya Hati hiyo, na kwamba haijawahi kupelekwa na kusajiliwa katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, Serikali hii ya CCM ililazimika kutoa kile ilichokiita nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano.
Hatuhitaji kuzungumzia tofauti kubwa ya sahihi ya Sheikh Karume iliyoko kwenye Hati hiyo na sahihi ya Sheikh Karume iliyoko katika Sheria mbali mbali alizosaini kama Rais wa Zanzibar na wakati mwingine kama kaimu Rais wa Jamhuri ya Muungano. Cha muhimu ni kwamba mgogoro juu ya Hati ya Makubaliano ya Muungano unathibitisha ukweli kwamba matokeo ya utamaduni huu wa kufichaficha nyaraka muhimu za nchi ni kwa wananchi kukosa imani na serikali iliyoko madarakani, kwa kuwa wananchi wanajenga hisia kwamba nyaraka hizo zinafichwa kwa sababu zina ushahidi wa maovu yaliyofanywa na serikali hiyo.
Kwa sababu hizi zote, kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa nyaraka za Muungano huu hadharani ili Watanzania waweze kuelewa historia halisi ya Muungano badala kuendelea kulishwa propaganda na TBC na kwenye majukwaa ya kisiasa ya CCM na Serikali yake! Vinginevyo, chochote kitakachosemwa na TBC na watawala katika majukwa yao ya kisiasa kuhusu Muungano huu hakitaaminika tena na wananchi wa Tanzania.
KIELELEZO CHA UMOJA NA MSHIKAMANO AU UNYONYAJI WA KIKOLONI?
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba ya Waziri Mkuu Bunge lako tukufu limeambiwa kwamba “Muungano huu ni wa kipekee na wa kupigiwa mfano duniani kote. Aidha, ni kielelezo kamili cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi....” Ni kweli kwamba Muungano huu ni wa kipekee kwa sababu haujawahi kuigwa na nchi nyingine zozote katika Afrika. Na kama Muungano huu ungekuwa wa ‘kupigiwa mfano duniani kote’, kama inavyodaiwa na Waziri Mkuu, basi kungekuwa na angalau nchi moja iliyoomba kujiunga katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Angalau kungekuwa na nchi zilizoiga mfano wa Muungano huu kwingineko Afrika na duniani kote.
Kwa kuwa hakuna nchi hata moja iliyowahi kuomba kujiunga nasi, na kwa kuwa hakuna nchi nyingine zilizoiga mfano wa Muungano huu, pengine huu ni muda muafaka wa kuhoji ukweli wa kauli kwamba Muungano huu ‘ni kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi’ wa Tanganyika na Zanzibar. Mzee Pius Msekwa, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Spika Emeritus wa Bunge hili tukufu, aliwahi kusema katika mada yake Hali ya Muungano kwa semina iliyofanyika Tanga miaka 20 iliyopita kwamba, muundo wa sasa wa Muungano huu umepelekea wengi kuamini kwamba Muungano huu ni kiini macho tu.
Hii ni kwa sababu, chini ya Muungano huu, Zanzibar ilikabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na ushuru, sarafu, nguvu kuu za kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa Tanganyika; na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya Muungano. Spika Emeritus Msekwa aliongeza kwamba kwa jinsi mambo yalivyo sasa, Zanzibar inaonekana kama vile ni ‘invited guest’ (mgeni mwalikwa) katika Muungano huu.
Naye msomi mashuhuri wa Kiafrika, Profesa Ali A. Mazrui katika makala yake ‘Imperialism after the Empire: Lessons from Uganda and Tanzania’, yaani ‘Ubeberu Baada ya Himaya: Funzo Kutoka Uganda na Tanzania’, iliyochapishwa katika gazeti la Kenya, The Sunday Nation, la Mei 22, 1994, alisema kwa sababu ya Muungano, Zanzibar imepoteza kila kitu chake muhimu, wakati Tanganyika imebadilika jina tu na kuwa Tanzania, huku ikiwa na mamlaka zaidi lakini ikibaki na Rais wake, nembo yake ya Taifa, wimbo wake wa Taifa na hata kiti chake katika Umoja wa Mataifa. Kama tunavyoonyesha katika Maoni haya, gharama ya kuyapuuza maneno haya ya watu hawa wazito imekuwa kubwa kweli kweli, hasa kwa Zanzibar.
MISAADA NA MIKOPO YA KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Ushahidi wa nyaraka ambazo zimewasilishwa kwenye Bunge lako tukufu na Serikali hii ya CCM unaonyesha kwamba Muungano huu ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji mkubwa ambao nchi ndogo ya Zanzibar imefanyiwa na nchi kubwa ya Tanganyika. Ni mfano wa jinsi ambavyo nchi moja kubwa ya Kiafrika inaweza kuigeuza nchi nyingine ndogo ya Kiafrika kuwa koloni lake. Kwa sababu maneno haya yanaweza kupotoshwa na wale ambao wamefaidika na uhusiano huu wa kikoloni kati ya Tanganyika na Zanzibar naomba kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo.
Kwa miaka mingi Zanzibar imelalamika kwamba inapunjwa katika mgawanyo wa mapato yanayotokana na fedha zinazotolewa na nchi wafadhili na taasisi za kimataifa kwa Jamhuri ya Muungano. Kwa sababu ya malalamiko hayo, mwaka jana Kamati ya Kudumu ya Bunge lako tukufu ya Katiba, Sheria na Utawala iliiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kwamba: “Utaratibu wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na fedha zinazotoka kwa wafadhili ni vyema ukaangaliwa upya kwa Serikali zote mbili yaani SMZ na SMT.” Aidha, Kamati ilishauri kwamba “Serikali itolee uamuzi mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha yaliyowasilishwa Serikalini tangu mwaka 2006 na kuwasilishwa tena mwaka 2010 kuhusu utaratibu wa mgao wa fedha za Serikali zote mbili.”
Serikali hii ya CCM imejibu maagizo haya ya Kamati kama ifuatavyo: “Serikali zetu mbili bado zinaendelea kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Pamoja ya Fedha. Aidha, kuhusu mgawanyo wa fedha zinazotoka kwa wafadhili, upo utaratibu wa mgawanyo wake ambapo, kwa upande wa misaada na mikopo ya kibajeti isiyokuwa na masharti maalum, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ... hupata gawio la asilimia 4.5.”
Mheshimiwa Spika,
Kauli hii ya Serikali ni ya uongo. Katika maelezo yake mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, aliitaarifu Kamati kwamba “Kwa mwaka wa fedha 2013/14, hadi kufikia mwezi Machi, 2014 SMZ imepata Gawio la Misaada ya Kibajeti (General Budget Support – GBS) shilingi 27,190,502,190.97/= kati ya shilingi 32,627,535,000/= zilizoidhinishwa na Bunge.” Hii ndio kusema kwamba kati ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge lako tukufu kama gawio la misaada na mikopo ya kibajeti kwa Zanzibar, ni asilimia 83 ndizo zilizolipwa hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, hili sio tatizo, kwani kwa mwelekeo wa takwimu hizi, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha, gawio lililoidhinishwa na Bunge lako tukufu linaweza kuwa limelipwa lote. Tatizo kubwa na la msingi ni kwamba gawio lililoidhinishwa na Bunge hili tukufu sio gawio halali kwa Zanzibar. Hii kwa sababu, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (MB.) Akiwasilisha Mapendekezo ya Mfumo wa Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2014/15 kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya tarehe 30 Aprili, 2014, mapato halisi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yanayotokana na misaada na mikopo nafuu ya nje ilikuwa shilingi bilioni 1,163 au trilioni 1.163.
Kama Zanzibar ingepatiwa asilimia 4.5 ya mapato hayo, kama inavyotakiwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Serikali hii ya CCM, basi kwa mwaka jana peke yake, gawio halali la Zanzibar la misaada na mikopo ya kibajeti lingekuwa shilingi bilioni 52.335. Badala ya kupatiwa shilingi bilioni 52.335 ambazo ni fedha zake halali, Zanzibar iliidhinishiwa shilingi bilioni 32.627 au asilimia 52 ya fedha zake halali. Fedha hizo ni sawa na asilimia 2.8 ya fedha zote za misaada na mikopo ya kibajeti kwa Jamhuri ya Muungano. Fedha zilizobaki, yaani shilingi trilioni 1.130 au asilimia 97.2 ya fedha zote za misaada ya kibajeti zimetumika na zitatumika Tanganyika. Kwa ushahidi huu wa nyaraka za Serikali hii ya CCM, kwa sababu ya Muungano huu, kwa mwaka jana peke yake Zanzibar iliibiwa shilingi bilioni 25.145 au asilimia 48 ya fedha zake halali za gawio la misaada na mikopo ya kibajeti.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mapendekezo yaliyoletwa kwenye Bunge lako tukufu na Serikali hii ya CCM, Zanzibar itaibiwa fedha nyingi zaidi kwa mwaka huu wa fedha 2014/15. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, kwa mwaka huu wa fedha,“fedha zitakazokwenda SMZ zinajumuisha shilingi 21,639,608,000.00 mgao wa misaada ya kibajeti....” Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha, ‘misaada na mikopo ya kibajeti’ kwa mwaka huu wa fedha itakuwa shilingi bilioni 992.170. Hii ina maana kwamba kwa mwaka huu wa fedha, Zanzibar itapata asilimia 2.18 tu ya fedha za misaada na mikopo ya kibajeti. Hii inaonyesha pia kwamba, kwa mwaka huu, fedha za misaada na mikopo ya kibajeti ambazo zitabaki na kutumika Tanganyika ni shilingi bilioni 970.531 au asilimia 97.82 ya fedha hizo.
Kama Serikali hii ya CCM ingeheshimu utaratibu wake wa asilimia 4.5 ya fedha hizo kwa Zanzibar, gawio halali la Zanzibar kutokana na fedha za misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka ujao wa fedha lingekuwa shilingi bilioni 44.647! Kwa maana hiyo, Serikali hii ya CCM inapendekeza kuilipa Zanzibar asilimia 48.47 ya fedha zake halali. Endapo Bunge lako tukufu litapitisha mapendekezo haya kama inavyoombwa na Serikali hii ya CCM, Zanzibar itaibiwa shilingi bilioni 23 au asilimia 51.53 ya fedha zake halali kwa mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge lako tukufu na iwaeleze Watanzania, na hasa Wazanzibari, kwa nini fedha halali za Zanzibar kutokana na misaada na mikopo ya kibajeti inayokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano hazijalipwa kwa mwaka jana wa fedha. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge lako tukufu na iwaeleze Watanzania, na hasa Wazanzibari, kwa nini inapendekeza kuipatia Zanzibar pungufu ya fedha zake halali kama gawio la misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka huu wa fedha.
Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilete mbele ya Bunge lako tukufu takwimu za fedha zote zilizopokelewa na Serikali kama misaada na mikopo ya kibajeti kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita na sehemu ya fedha hizo zilizolipwa kwa Zanzibar kama gawio lake katika kipindi hicho. Takwimu hizo ni muhimu ili Watanzania, na hasa Wazanzibari, waweze kufahamu kama Zanzibar imekuwa ikipata sehemu yake halali ya mapato ya Jamhuri ya Muungano yanayotokana na misaada na mikopo ya kibajeti. Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaka Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule ya Bunge hili itakayochunguza mgawanyo wa mapato yanayotokana na misaada na mikopo ya kibajeti kati ya Tanganyika na Zanzibar ili kupata ukweli juu ya uhalali wa malipo ya mapato hayo kwa Zanzibar.
MISAADA NA MIKOPO ISIYOKUWA YA KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Misaada na mikopo ya kibajeti sio eneo pekee ambapo Zanzibar inanyonywa na Tanganyika kwa sababu ya Muungano huu. Ukweli ni kwamba hali ni mbaya zaidi kuhusiana na fedha za misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti. Hapa pia takwimu za Serikali hii ya CCM zinatisha na kusikitisha. Hivyo, kwa mfano, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha, kwa mwaka wa fedha 2013/14 fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikijumuisha misaada na mikopo ya Basket Fund na misaada na mikopo ya miradi zilikuwa shilingi trilioni 2.692 au bilioni 2,692. Fedha hizi zote zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Tanganyika. Hapa Zanzibar haikupata kitu chochote!
Maelezo ya Waziri wa Fedha yanaonyesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2014/15, misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti kutoka nje inatazamiwa kuwa shilingi bilioni 2,019.43 au trilioni 2.019. Hizi zote ni fedha zitakazotumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Tanganyika. Hapa pia Zanzibar haitapata kitu chochote. Ni muhimu kwa Bunge lako tukufu kukumbuka kwamba, kwa sababu ya Muungano huu, Zanzibar imenyang’anywa mamlaka ya kuomba mikopo au misaada kutoka nje bila kwanza kupata kibali cha Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano, aka Wizara ya Fedha ya Tanganyika. Sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka kujua unyonyaji na wizi huu wa fedha za Wazanzibari utakomeshwa lini. Aidha, sisi tulio kizazi cha Muungano huu tunataka kuambiwa kama mgawanyo wa aina hii wa mapato yanayokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano ndio kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar ulioletwa na Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Zanzibar haipati stahili yake ya mapato yanayopatikana kwa jina la Jamhuri ya Muungano kutoka vyanzo vya nje, bali pia fedha zinazopatikana kutokana na mambo ya Muungano zinatumika kwa mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika. Moja ya matokeo ya mjadala wa katiba wa mwaka 1983/84 uliopelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Alhaj Aboud Jumbe ni kuingizwa kwa Sura ya Saba inayohusu ‘Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano’ katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1984, ibara mpya ya 133 ya Katiba iliweka masharti kwamba “Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza ‘Akaunti ya Pamoja ya Fedha ... ambamo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili kwa kiasi kitakachoamuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha ... kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano.”
Aidha, ibara ya 134 iliweka masharti ya kuwa na Tume ya Pamoja ya Fedha yenye majukumu ya“kuchambua mapato na matumizi yanayotokana na, au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano na kutoa mapendekezo kwa Serikali mbili kuhusu mchango na mgawo wa kila mojawapo ya Serikali hizo.” Majukumu mengine ya Tume hiyo ni “kuchunguza ... mfumo wa shughuli za fedha kwa Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali mbili.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa miaka thelathini tangu kupitishwa kwa Mabadiliko ya Tano ya Katiba, masuala ya Tume ya Pamoja ya Fedha na Akaunti ya Pamoja ya Fedha yamekuwa mojawapo ya kile kinachoitwa ‘Kero za Muungano’ ambayo ufumbuzi wake umeshindikana. Kwa mfano, licha ya Katiba kuelekeza kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha, sheria ya kuunda Tume hiyo, yaani Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha, ilipitishwa miaka kumi na mbili baadaye, yaani mwaka 1996.
Baada ya hapo Tume yenyewe iliundwa rasmi mwaka 2003, yaani miaka saba baada ya kutungwa kwa sheria na miaka 19 tokea Katiba iweke masharti ya kuundwa kwa Tume hiyo. Kwa upande wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha, leo ni mwaka wa thelathini tangu Katiba kuelekeza Akaunti hiyo kufunguliwa na bado haijafunguliwa. Kutokana na kushindikana kufunguliwa huko, kwa miaka yote hii, bajeti ya Muungano imekuwa ndio bajeti ya Tanganyika, kinyume na maelekezo ya Katiba.
Mwaka 2006 Tume ya Pamoja ya Fedha iliajiri wataalamu waelekezi kutoka kampuni kimataifa ya uhasibu ya PriceWaterhouseCoopers kuangalia suala la gharama na mgawanyo wa fedha za Muungano. Wataalamu hao walifanya uchambuzi halisi wa mambo yapi ni ya Muungano na yapi ni ya Tanganyika na yapi ni ya Zanzibar na gharama za uendeshaji wa kila moja. Baada ya orodha kupatikana, watafiti hao walitafuta matumizi halisi ya bajeti ya vifungu hivyo kwa muda wa kiasi cha miaka 10 iliyopita.
Watafiti wa PriceWaterhouseCoopers walikwenda mbali zaidi ya hapo na kukusanya mapato yote kwa kila kifungu cha mambo ya Muungano halisi. Mwishowe, wakalinganisha iwapo mapato hayo yanakidhi matumizi ya Muungano au yana upungufu. Taarifa ya uchambuzi wa PriceWaterhouseCoopers ilitolewa kama Mapendekezo ya Tume Kuhusu Vigezo vya Kugawana Mapato na Kuchangia Gharama za Muungano ya mwezi Agosti 2006.
Taarifa ya Tume ya Pamoja ya Fedha inaonyesha hali ya kusikitisha kuhusu mapato na matumizi ya fedha za Muungano, hasa kwa upande wa Tanganyika. Ili kupata picha kamili ya hali halisi ilivyo, tunaomba kunukuu sehemu ya Taarifa hiyo in extenso, kwenye ukurasa wake wa 18: “Uchambuzi unaonyesha kuwa mapato yanayotokana na vyanzo vya Muungano yanakidhi matumizi ya Muungano na kuwa na ziada ya kutosha. Takwimu zinaonyesha kuwa kiasi kidogo cha mapato hayo kimekuwa kinagharimia matumizi ya Muungano. Kwa mfano, uwiano huu ulikuwa ni (shilingi bilioni 360.679 kati ya (shilingi bilioni 1,030.513) sawa na asilimia 35 mwaka 1999/2000, (shilingi bilioni 468.450) kati ya (shilingi bilioni 1,801.733) sawa na asilimia 26 mwaka 2002/03, na (shilingi bilioni 636.078) kati ya (shilingi bilioni 2,271.710) sawa na asilimia 28 mwaka 2003/04.
“Uchambuzi unaonyesha kuwa kiasi kikubwa cha ziada ya mapato ya Muungano kimekuwa kinatumika kugharimia mambo yasiyo ya Muungano. Viwango hivi kwa mwaka 1999/2000 vilikuwa ni (shilingi bilioni 39.822) sawa na asilimia 5.9 kwa (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) na (bilioni 631.714) sawa na asilimia 94.1 kwa Tanzania Bara. Viwango hivi vilibadilika kwa kiasi kikubwa kwa mwaka wa fedha 2003/04 ambapo kwa (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) kilishuka hadi (shilingi bilioni 37.053) sawa na asilimia 2.3, na (shilingi bilioni 1,588.494) sawa na asilimia 97.7 kwa (Serikali ya Muungano wa Tanzania).”
Takwimu za utafiti wa PriceWaterhouseCoopers zinaonyesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2003/2004 pekee, matumizi halisi kwa vifungu vya Muungano yalikuwa shilingi bilioni 537.258 ambayo ni asilimia 20 tu ya bajeti yote ya Serikali ya Muungano kwa mwaka huo. Mapato halisi ya vyanzo vya mapato vinavyotokana na mambo ya Muungano kwa mwaka huo yalikuwa ni shilingi bilioni 1,030.826, au takriban shilingi trilioni 1.030. Kwa maana nyingine, mapato na matumizi ya fedha zinazotokana na vyanzo vya mambo ya Muungano yaliacha ziada ya shilingi bilioni 493.567 kwa mwaka huo mmoja. Ziada hii ni nje ya mapato yaliyotokana na misaada na mikopo kutoka nje, na ilitumika kwa shughuli za maendeleo za Tanganyika zisizo za Muungano.
Kwa sababu Tanganyika imekuwa inafaidika sana na utaratibu huu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano - ambayo kiuhalisia ni Serikali ya Tanganyika iliyovaa joho la Muungano – imekataa kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha kwamba uwekwe utaratibu utakaowezesha kutenganisha mapato na matumizi ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Miaka nane tangu mapendekezo hayo yatolewe mwaka 2006, “Serikali zetu mbili”, kwa maneno ya Mh. Samia Suluhu Hassan, “bado zinaendelea kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Pamoja ya Fedha.”
Mheshimiwa Spika,
Kero nyingine kubwa ya Muungano huu na ambayo ina umri karibu sawa na Muungano wenyewe inahusu hisa za Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki kabla ya Bodi hiyo kuvunjwa mwaka 1965 na Benki Kuu ya Tanzania kuanzishwa. Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Suluhu Hassan, hisa za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ni mojawapo ya “kero zilizobaki katika orodha ya mambo ya kutafutiwa ufumbuzi....” Kufuatana na maelezo hayo, “masuala ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu yapo katika ngazi ya Mawaziri wa Fedha wa (Serikali ya Jamhuri ya Muungano) na (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) kwa hatua za majadiliano.”
Alipohojiwa juu ya hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwezi Januari 2013, Waziri huyo huyo aliiambia Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwamba: “Katika Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano kilichofanyika tarehe 14 Januari 2013 imeelezwa kwamba Mawaziri wa Fedha wa SMT na SMZ wamepatiwa nyaraka maalum zenye taarifa za siri na wamekubaliana kujadili suala hili mwezi Februari, 2013 baada ya kuzipitia nyaraka hizo.”Kwa vile bado mawaziri wanajadiliana, kama tulivyosema mwaka jana, “sio tu kwamba Wazanzibari hawajui ni kiasi gani cha fedha zao zilichukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kufuatia kuvunjwa kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, bali pia hawana uhakika watazirudishiwa lini!”
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile fedha za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu zilichukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano baada ya masuala ya fedha, sarafu na Benki Kuu kufanywa kuwa mambo ya Muungano mwaka 1965, sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tuna haki ya kuambiwa ukweli kwanini Serikali hii ya CCM imeshindwa kurudisha fedha hizo kwa Wazanzibari kwa takriban miaka hamsini tangu fedha hizo zinyakuliwe na Serikali ya Jamhuri ya Muungano aka Serikali ya Tanganyika? Tunahitaji kuelezwa Serikali hii ya CCM inahitaji muda wa miaka mingapi mingine ili iweze kurudisha fedha za watu na kuwaepusha Watanganyika na laana ya wizi wa fedha za Wazanzibari?
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au Wazanzibari wenyewe katika umoja wao, wana haki ya kutumia njia yoyote ile watakayoona inafaa, ikiwamo kufungua kesi za madai katika mahakama za ndani au mahakama za kimataifa, kudai fedha zake zote halali ambazo zimeibiwa na Tanganyika kwa kutumia kivuli cha Muungano katika kipindi chote cha miaka hamsini ya Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa vyovyote vile, takwimu hizi zinaonyesha kwamba, kwa sababu ya Muungano huu, uhusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni uhusiano wa kinyonyaji. Kwa sababu hiyo, huu ni uhusiano wa kikoloni. Ni uhusiano kati ya ‘himaya’ ya Tanganyika na ‘koloni’ lake la Zanzibar. Himaya za kikoloni huwa zinadhibiti masuala yote ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, uraia, kodi, fedha, sarafu na benki kuu ya makoloni yao. Na himaya za kikoloni huwa zinatumia nguvu na udhibiti wao wa masuala haya kuyanyonya makoloni yao kiuchumi, kuyadidimiza kijamii na kuyatawala kisiasa. Hivi ndivyo ambavyo imekuwa kwa mahuasiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu kuzaliwa kwa Muungano huu tarehe 26 Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 20 Aprili, 1968, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo wakati akihojiwa na gazeti la The Observer la London, Uingereza: “If the mass of the people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason of their own, decide that the Union was prejudicial to their existence, I could not bomb them into submission.... The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members was withdrawn.” Yaani,“endapo umma wa wananchi wa Zanzibar wataamua, bila kurubuniwa kutoka nje na kwa sababu zao wenyewe, kwamba Muungano unaathiri kuendelea kuwepo kwao, sitaweza kuwalazimisha kwa kuwapiga mabomu.... Muungano hautaendelea kuwepo pale ridhaa ya washirika wake itakapoondelewa.”
Miaka 45 baada ya kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere, Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema yafuatayo katika Maoni aliyoyatoa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 13 Januari, 2013: “Mfumo (wa Muungano) uliopo sasa hauinufaishi Zanzibar na hivyo haukubaliki kwa Wazanzibari. Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana sana. Wakati umefika tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi.”
Nalo Baraza la Wawakilishi Zanzibar, katika maoni yake kwa Tume ya tarehe 5 Februari, 2013, limetaka ‘kuwa na Muungano wa dhati’, yaani “... Muungano wa kweli, hata kama ni kwa maeneo machache, kwa dhati ya wanasiasa na Watanzania kwa ujumla.” Kwa mujibu wa Baraza hilo, Muungano ‘wa dhati’ na ‘wa kweli’ ni ule ambao kuna “... Mamlaka ya Zanzibar huru na Mamlaka ya Tanganyika huru ndani ya Muungano, (na) Mamlaka ya Muungano iwekwe wazi – maeneo yake, uwezo au nguvu zake, na utendaji wake. Mambo yote hayo yawekwe wazi na mipaka yake.”
Aidha, Baraza la Wawakilishi limependekeza kwamba “rasilmali za Muungano ziwe ni milki ya pande mbili za Muungano; na rasilmali hizo ndio zitumike katika uendeshaji wa Mamlaka za Muungano. Ugawaji wa rasilmali ufanywe kwa uwiyano maalum utakaokubaliwa kwa pamoja na pande mbili za Muungano.”
Hata kama baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar baadaye waliyakana maneno yao haya walipofika mbele ya wakubwa wao wa Tanganyika wakati wa vikao vya Bunge Maalum hapa Dodoma, haya sio maneno ya kupuuza hata kidogo kwa sababu yanathibitisha kwamba hata wale Watanzania wachache, kama wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambao wamefaidika kwa kupata nafasi za uongozi kwa sababu ya Muungano, hawauoni Muungano huu kama kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo wao. Kuyapuuza maneno haya ni kujenga misingi imara na hakika ya Muungano huu kuvunjika.
NCHI MOJA AU NCHI MBILI?
Mheshimiwa Spika,
Kuna propaganda na uongo mwingine juu ya Muungano huu ambayo imeenezwa sana katika kipindi hiki cha nusu karne ya uhai wake. Propaganda hii inahusu kile kilichozaliwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano, yaani Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Baada ya jina la Jamhuri hiyo kubadilishwa kuwa Tanzania tarehe 28 Oktoba, 1964, ilizaliwa dhana kwamba Makubaliano ya Muungano yaliua nchi za Tanganyika na Zanzibar na kuanzisha ‘nchi moja’ ya Tanzania. Dhana hii imetumika, katika miaka hamsini ya Muungano huu, kuhalalisha ukiukwaji wa matakwa ya Makubaliano ya Muungano kwa kutumia dhana nyingine ya ‘kuimarisha Muungano.’ Dhana hizi mbili ndio msingi wa nyongeza zote za mambo ya Muungano, na ndio sababu kubwa ya kuporomoka kwa uhuru na mamlaka ya Zanzibar katika kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika,
Dhana kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano iliua nchi mbili na kuzaa nchi moja ya Tanzania ni dhana potofu na isiyokuwa na msingi wowote katika Hati yenyewe. Kwanza, Hati ya Makubaliano ya Muungano ilitamka wazi kwamba sheria zilizokuwepo Tanganyika na Zanzibar kabla ya Muungano zitaendelea kutumika ‘katika nchi zao’ hadi hapo zitakaporekebishwa ili kutilia nguvu Muungano na Hati za Muungano; au sheria mpya zitakapotungwa na mamlaka husika au kutolewa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya utekelezaji wa Mambo ya Muungano kwa upande wa Zanzibar.
Pili, vifungu mbali mbali vya Katiba zilizofuatia Makubaliano ya Muungano ziliweka wazi kwamba Tanganyika na Zanzibar hazikuuawa na Makubaliano ya Muungano. Hivyo basi, hata baada ya mabadiliko ya jina kwenda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba na sheria mbali mbali ziliendelea kutumia jina la Tanganyika na Zanzibar. Kwa mfano, Sheria ya Kuongeza Muda wa Kuitisha Bunge la Katiba, 1965, iliyosainiwa na Rais Nyerere tarehe 24 Machi, 1965, inataja, katika vifungu vyote vitatu, ‘Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Aidha, Sheria ya Kutangaza Katiba ya Muda ya Tanzania ya tarehe 11 Julai, 1965, ilitangaza kwamba ‘Tanzania ni Jamhuri Huru ya Muungano’; kwamba eneo lake ni “... eneo lote la Tanganyika na Zanzibar ...” na kwamba chama kimoja cha siasa “... kwa Tanganyika kitakuwa Tanganyika African National Union (TANU)....” Kwa wakati wote wa uhai wake, Katiba ya Muda haikuwahi kutamka kuwa Tanzania ni nchi moja. Badala yake, ibara ya 27(1) ya Katiba hiyo iliyokuwa inahusu sifa za kuchaguliwa kuwa mbunge ilitamka wazi kwamba: “Raia yeyote wa Tanganyika ambaye amefikisha umri wa miaka ishirini na moja na ni mwanachama (wa TANU) atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo....”
Kwa upande wake, licha ya kuanza kutumia jina la Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa mara ya kwanza, Toleo la Kwanza la Katiba ya sasa ya Muungano lilitamka kwamba Tanzania ni ‘Jamhuri ya Muungano.’ Hapa pia hapakuwa na tamko la ‘nchi moja.’
Mheshimiwa Spika,
Maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya sasa ya Muungano kwamba “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” yaliingia katika kamusi ya kikatiba na kisiasa ya nchi hii kufuatia ‘kuchafuka kwa hali ya kisiasa ya Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe. Kufuatia hali hiyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa ambayo, pamoja na mengine, yalitangaza kuwa “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.”Kwa sababu ya upinzani mkubwa wa Wazanzibari, Marekebisho hayo ya Katiba yaliondoa pia maneno ‘Tanzania Visiwani’ na kuweka ‘Tanzania Zanzibar’ badala yake. Maneno ‘Tanzania Bara’ yalibaki kama yalivyowekwa mwaka 1977.
Kwa maana hiyo, dhana ya Tanzania kama nchi moja haijatokana na Makubaliano ya Muungano bali ilitokana na siasa za Muungano, yaani mvutano kati ya viongozi wa Tanganyika wakiwa wamevalia joho la Jamhuri ya Muungano na viongozi wa Zanzibar waliotaka uhuru zaidi kwa nchi yao. Pili, dhana hiyo haina umri mkubwa sana kuliko inavyodhaniwa, kwani iliingia kwenye Katiba mwaka 1984, miaka thelathini iliyopita, na miaka ishirini baada ya Muungano.
MUUNGANO USIO WA USAWA
Mheshimiwa Spika,
Tangu mwanzo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuwa Muungano wa usawa. Huu ni Muungano ulioipa Tanganyika – ikiwa imevalia koti la Jamhuri ya Muungano - mamlaka ya kuingilia uhuru na mamlaka ya Zanzibar. Hii inathibitishwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano yenyewe. Kwanza, kwa kutamka kwamba katika kipindi cha mpito “Katiba ya Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Katiba ya Tanganyika...”, ni wazi kwamba Mshirika wa Muungano aliyekuwa na nguvu katika Muungano huu ni Tanganyika.
Pili, kwa kuweka orodha ya mambo 11 ya Muungano, ni wazi kwamba Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka juu ya masuala hayo na mamlaka hayo yalihamishiwa kwa Tanganyika ikiwa imevaa koti la Jamhuri ya Muungano. Kwa maana hiyo, Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka yake juu ya masuala ya nchi za nje, ulinzi, polisi, mamlaka ya hali ya hatari, uraia, uhamiaji, biashara ya nje na mikopo na masuala mbali mbali ya kodi. Hati ya Makubaliano ya Muungano yenyewe inasema wazi kwamba “Bunge na Serikali (ya Jamhuri ya Muungano) litakuwa na mamlaka kamili kwenye mambo hayo kwa Jamhuri ya Muungano na, kwa nyongeza, mamlaka kamili kwa ajili ya mambo mengine yote ya na kwa ajili ya Tanganyika.”
Tatu, kwa kutangaza kwamba rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mwalimu Nyerere na Makamu wa kwanza wa Rais atakuwa Sheikh Abeid Karume; na kwa kutangaza kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa majukumu yake ya kiutendaji kuhusu Zanzibar, ni wazi kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano ilithibitisha nafasi ya chini (subordinate position) ya Zanzibar katika Muungano.
Nne, kwa kuzifanya alama za utaifa (national emblems) za Tanganyika kuwa ndio alama za taifa za Jamhuri ya Muungano, kuna-emphasize superior position ya Tanganyika ndani ya Muungano na subaltern position ya Zanzibar katika Muungano huu. Ukweli huo huo unahusu masuala ya kuzifanya taasisi na watumishi wa Serikali ya Tanganyika kuwa ndio taasisi na watumishi wa Jamhuri ya Muungano.
Tano, hata kwa kuangalia watu ambao wamewahi kupata fursa ya kuongoza Jamhuri ya Muungano, ni wazi kwamba Watanganyika ndio wamekuwa mabwana na Wazanzibari wamefanywa watwana katika masuala ya haki za kiutawala. Hivyo, kwa mfano, katika kipindi cha miaka hamsini ya Muungano huu, ni Mzanzibari mmoja tu ndiye aliyepata fursa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa miaka kumi kati ya miaka hamsini hiyo.
Kwa utaratibu huo huo, tokea mwaka 1964, Zanzibar haijawahi kutoa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi au Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Zote hizi ni taasisi za Muungano. Aidha, Zanzibar imewahi kutoa Waziri Mkuu mmoja tu, tena kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, na Jaji Mkuu mmoja tu katika kipindi hicho cha nusu karne ya Muungano huu. Vile vile, katika Diplomatic Corps, kwa sasa kuna Wazanzibari wawili tu ambao ni mabalozi wa Tanzania nchi za nje kati ya mabalozi 32 wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje.
Mheshimiwa Spika,
Hata Bunge lako tukufu lina rekodi mbaya katika masuala haya. Hivyo, kwa mfano, katika miaka yote ya Muungano, hakuna Mzanzibari ambaye amewahi kushikilia nafasi ya Spika au Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Aidha, licha ya Kanuni za Bunge lako tukufu kuruhusu kufanyika kwa vikao vya Kamati zake za Kudumu nje ya Dodoma, yaani Dar es Salaam na/au Zanzibar; na licha ya Kanuni kuruhusu Mikutano ya Bunge kufanyika nje ya Dodoma ikiwa ‘itaelekezwa vinginevyo’, hakuna Kamati hata moja ya Bunge hili tukufu ambayo imewahi kufanya vikao vyake Zanzibar na haijawahi kutokea Bunge hili likaelekezwa kufanya Mikutano yake nje ya Tanganyika!
KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Baada ya nusu karne ya Muungano wa aina hii, wananchi wa Tanganyika na, hasa wa, Zanzibar hawako tayari kuendelea na utaratibu huu wa kinyonyaji na kikandamizaji. Wananchi wanataka mabadiliko ya msingi ya muundo wa Muungano na uendeshaji wake. Wananchi wanataka kusikilizwa juu ya Muungano. Wananchi wanataka kufanya maamuzi kuhusu kama wanataka kuendelea na Muungano na, kama jibu ni ndiyo, muundo wa Muungano huo.
Wakati wa mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum, Kamati nyingi zilishindwa kufanya maamuzi kwa sababu ya kukosa uungwaji mkono wa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Kamati kutoka Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wajumbe kutoka Zanzibar. Kama hali ni hiyo katika Bunge Maalum licha ya Bunge hilo kujazwa wajumbe wengi wa CCM kutoka kundi la 201, hali ni mbaya zaidi nje ya Bunge Maalum na nje ya Bunge lako tukufu. Nje ya mabunge haya, watu wengi, hasa Wazanzibari ambao ndio wamekuwa waathirika wakubwa wa Muungano huu katika nusu karne ya maisha yake, wananchi wengi hawataki tayari kuendelea na Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Katika mazingira haya, namna muafaka ya kutoka katika constitutional impasse inayokuja mbele yetu, ni kuwauliza wananchi wa Tanganyika na Zanzibar – kwa kutumia kura ya maoni - kama bado wanataka kuendelea na Muungano huu. Na kama jibu lao litakuwa ni ndiyo, basi wananchi waamue, katika kura hiyo, ni muundo gani wa Muungano wanautaka. Miaka hamsini ya watawala kuamua masuala haya muhimu peke yao inatosha. Huu ni wakati muafaka kwa wananchi kufanya maamuzi haya makubwa kwa maisha yao na kwa nchi zao mbili. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawataka wabunge wa Bunge lako tukufu wawe kwenye upande sahihi wa historia, yaani upande wa wananchi katika jambo hili.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Katika kuhitimisha maoni haya, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wakuu wa vyama vyetu vitatu vinavyounda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kufanya maamuzi ya kuendeleza ushirikiano ulioanzia ndani ya Bunge Maalum, kwenye Bunge lako tukufu. Wananchi wetu wanataka mabadiliko ya msingi ya utawala wa nchi zetu mbili na usimamizi wa rasilmali zake. Kama ilivyokuwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ndani ya Bunge Maalum, ndivyo wananchi wanavyotutazamia kuendesha shughuli zetu ndani ya Bunge hili tukufu. Historia itatuhukumu vikali endapo tutashindwa kukamata fursa hii ya kihistoria katika nchi zetu mbili.
Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.


---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company