Watu wasiopungua 30 wameuawa kufuatua mlipuko wa bomu lililotegwa na magadi katika kijiji kimoja nchini Nigeria katika Jimbo la Borno la kaskazini mashariki. Duru zinaarifu kuwa watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la Boko Haram walitekeleza hujuma hiyo iliyolenga daraja linaloziunganisha Nigeria na Cameroon nje kidogo ya kijiji cha Gamboru Ngala Alkhamisi usiku. Hayo yamejiri baada ya maafisa wa Nigeria kusema kuwa siku ya Jumatano tarehe 7 mwezi huu wa Mei magaidi wa kundi la Boko Haram walikishambulia kijiji hicho hicho na kuwaua watu wasiopungua 300.
Hujuma hizo zinakuja huku kukiandaliwa oparesheni maalumu nchini Nigeria kwa lengo la kuwanusuru wasichana wa shule wapatao 276 ambao walitekwa nyara hivi karibuni na magaidi wa Boko Haram katika Jimbo la Borno.
Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Maelfu ya watu wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi hilo lianzishe uasi mwaka 2009. Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.