Rais Salva Kiir na Kiongozi wa waasi Riek Machar wakitia sahihi mkataba wa kusitisha vita kwa masaa 24 nchini humo.
Rais wa Sudan kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi nchini humo Riek Machar wametia sahihi mkataba wa kusititisha vita chini ya masaa 24.
Wawili hao pia wamekubaliana kuruhusu msaada wa kibinaadamu kungia nchini humo mbali na kubuniwa kwa serikali ya mpito.
Mazungumzo hayo yaliofanyika katika mji mkuu wa Ethiopi,a Addis Ababa yalisimamiwa na viongozi wa Shirika la IGAD pamoja na waziri mkuu nchini Ethiopia Hailemariam Desalegn ambaye ndio mwenyekiti wake.
Mwandishi wa BBC katika mazungumzo hayo amesema inatarajiwa kuonekana iwapo mkataba huo utaafikiwa kufuatia tofauti za kikabila zilizopo nchini humo ambapo maelfu ya watu wameuawa na zaidi millioni moja wengine kuachwa bila makao tangia mzozo huo uanze mnamo mwezi Disemba.
Wakati huohuo waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry ambaye alishinikiza mkataba huo amefurahishwa na hatua hiyo.
katika taarifa yake Kerry amemuagiza rais Salva kiir na Riek Machar kuchukua hatua za haraka ili kuafikia mkataba huo na kuhakikisha kuwa vikundi vilivyojihami katika pande zote mbili vinaafikia mkataba huo.
Mpango huo unajiri baada ya ripoti ya umoja wa mataifa kuzishtumu pande zote mbili kwa kutekeleza uhalifu dhidi ya binaadamu ikiwemo mauaji ya kimbari,utumwa wa kingono pamoja na ubakaji wa kimakundi.
Afisa anayesimamia maswala ya kibinaadamu katika umoja wa mataifa Navi Pillay amesema kuwa ripoti hiyo ina maswala mengi yanayoweza kuchochea mauaji ya kimbari.