Pierre René-Worms/RFI
Na RFI
Wanajeshi wa tano wa kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Mali (Minusma) kutoka Burkina Faso wameuawa Alhamisi wiki hii katika shambulio lililoendeshwa na kundi la watu wenye silaha kaskazini mwa Mali.
Kwa mujibu wa vyanzo viliyonukuliwa na shirika la habari la Ufaransa AFP, wanajeshi hao wa tano wameuawa katika shambulio la kuvizia dhidi ya msafara wa magari ya kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Mali (Minusma) kwenye barabara iliyo kati ya miji ya Goundam na Tombouctou.
Kundi la wapiganaji wa kiislamu la Aqmi lenye mafungamano na Al Qaeda limekiri kuhusika na shambulio hilo.
Kundi hili limekua likiendesha mashambulizi mbalimbali kaskazini mwa Mali.
Katikati mwa mwezi uliyopita askari polisi mmoja wa Mali aliuawa na watu wawili walijeruhiwa katika shambulio lililoendeshwa dhidi ya kijiji kimoja kusini mwa Mali.
Magari na pikipiki vilichomwa moto katika shambulio hilo. Wanajihadi walinyooshewa kidole kuhusika na shambulio hilo, kwani inasemekana kuwa walipandisha bendera yao katika kambi moja ya kijeshi katika moja ya eneo la kusini mwa Mali kabla ya kutoweka.
Mwezi huo huo kuliripotiwa mapigano makali kati ya jeshi la Mali na wapiganaji wa kijihadi katika mji huo wa Sikasso, maafisa wakuu wa Jeshi la nchi hiyo Walithibitisha,
Ni kwa mara ya kwanza wanajihadi wanahusishwa katika shambulio lililoendeshwa katika jimbo la Sikasso linalopakana na Côte d’Ivoire na Burkina-Faso.