MISWADA YA GESI YAZUA KIZAAZAA

SPIKA wa Bunge jana alilazimika kuahirisha shughuli za Bunge kutokana na baadhi ya wabunge kukataa miswada mitatu isisomwe na kujadiliwa kwa pamoja chini ya hati ya dharura.

Wakati Spika akisema kuwa utaratibu huo ni wa kawaida na umekuwa ukifuatwa kwenye vikao vingine vya Bunge vilivyopita, Kambi ya Upinzani ilikataa maelezo hayo, kwa madai kuwa ni ukiukwaji wa kanuni unaolenga kufunika kombe ili mwanaharamu apite.

Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kuisha saa 4:00 asubuhi jana, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo wa Spika, akieleza kuwa, karatasi yenye maelekezo ya shughuli za Bunge jana ilikuwa imebebanishwa miswada mingi kinyume na taratibu.

Mnyika alianza kwa kusoma kanuni kadhaa, na kuulizwa na Spika alikuwa akitaka nini kati ya mwongozo au taarifa, kwa sababu hakueleza kama anavyopaswa kufanya, ndipo aliposema; “Ninaomba mwongozo, na ninautaka sasa hivi, wala sio wakati mwingine, kwa sababu, inavyoonekana katika orodha ya miswada kwenye karatasi hii (aliionesha) ya shughuli za Bunge (order paper), imebebanishwa minne ifanyiwe kazi kwa wakati mmoja, jambo ambalo ni tofauti na ukiukwaji wa kanuni”, alisema.

Miswada iliyokuwa kwenye orodha ya shughuli za Bunge jana ni Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015.

Kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alisimama kuomba muongozo kwa sababu katika orodha ya shughuli hizo ilionesha kuwa baada ya maswali na majibu kulikuwa na miswada ya serikali, ambapo ilionesha ni kusomwa kwa mara ya pili na kusomwa mara ya tatu.

Alisema miswada ya mafuta iliwasilishwa kwa hati ya dharura, hivyo kudai kanuni zimekiukwa, jambo ambalo Spika Makinda alilipinga na kusema hakuna kanuni iliyokiukwa, hali iliyofanya wabunge wa upinzani kusimama na hivyo Spika kusitisha shughuli hizo.

Mnyika alisema, “Pamoja na kuletwa kwa hati ya dharura ifanyiwe kazi yote leo hii (jana), hatua hiyo inakiuka makubaliano ya kamati ya uongozi iliyokaa Juni 29, katika ukumbi wa Msekwa katika viwanja vya Bunge hili”.

Alisema kilichotakiwa ni kukamilisha shughuli ya kupitisha au kutopitisha muswada wa Kuwalinda watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi, ulioachwa kiporo juzi, ndipo kazi nyingine zifuate.


Akijibu hoja yake, Spika Makinda alisema: “Kwanza ninaomba ufute kauli yako ya kuniamrisha nikupe mwongozo leo hii kwa sababu huna mamlaka ya kufanya hivyo, vinginevyo sitajibu kitu, nitakaa kimya”.

Mnyika alifanya kama alivyoelekezwa na ndipo Spika alipojibu kuwa kinachofanywa katika kikao hicho cha Bunge si uvunjaji wa kanuni, bali ni utaratibu ambao umekuwa ukifuatwa hata kwenye vikao vingine vya Bunge hilo.

“Kinachoonekana kwenye karatasi hiyo ni miswada na itafanyiwa kazi mmoja baada ya mwingine kama kawaida. Hakuna kanuni iliyo vunjwa hapo na hakuna ukiukwaji wa makubaliano uliofanyika,” Makinda alisema na ndipo Lissu aliposimama kama Mnyika na kuwaonesha ishara ya kusimama wabunge wengine wa upinzani, ambao walitii.

“Kutokana na vurugu hiyo ya muda mfupi na majibishano yaliyomchukiza Spika aliamua kusema: Nina ahirisha kikao hiki hadi baadaye,” alisema Spika.

Bunge lilirejea tena jioni na kuendelea kupitisha muswada wa kuwalinda watoa taarifa.

Wakati Spika akitoka nje, baadhi ya wabunge wa upinzani walisikika wakitoa maneno kuwa safari hii hawatatoka nje ya Bunge kuwapa mwanya wengine waendelee kujadili miswada, bali watakuwepo ndani ya ukumbi huo wakiwa wamesimama tu kuzuia chochote kisiendelee bila kufikia makubaliano.

Rage atoa tuhuma nzito

Mbunge Tabora Mjini, Ismail Rage (CCM) aliwatuhumu baadhi ya wafanyabiashara wa madini, mafuta na gesi kwamba wameingiza mkono katika suala la miswada ya mafuta na gesi kwa kuwatumia baadhi ya wabunge ili miswada hiyo isiwasilishwe bungeni, huku serikali ikisema ikikwama ni hasara kwa Watanzania.

Rage alitoa kauli hiyo kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa jana, muda mfupi baada ya Spika wa Bunge, Anna Makinda kusitisha shughuli za Bunge baada ya kipindi cha maswali na majibu asubuhi, kutokana na wabunge wa upinzani kugomea uwepo wa miswada hiyo katika orodha ya shughuli za bunge za jana.

Lakini akizungumzia kadhia hiyo, Rage alisema ina msukumo wa baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta, madini na gesi ambao hawataki miswada hiyo iwasilishwe bungeni na kupitishwa kuwa sheria kwa sababu ina mambo mengi yenye maslahi kwa nchi.

“Siku zote tunapiga kelele tuone mikataba ya madini, gesi na mafuta tunataka iwe wazi, leo Serikali inaleta bungeni sisi tunapinga, hapa kuna namna, tunajua. Wapo baadhi ya wabunge wa upinzani na wengine hata wa CCM wanatumika kwa maslahi ya wafanyabiashara. “Wapo baadhi ndani ya CCM hawajui wanafuata mkumbo na baadhi wanatumika, lakini pia wapo wa upinzani wanafuata mkumbo na wengine nao wanatumika, hili ni jambo kubwa zaidi ya wengi wanavyofikiri,” alisema.

“Miswada hii ikipitishwa na kuwa sheria itaweka uwazi katika leseni na mikataba ya madini, gesi na mafuta, jambo ambalo ni jema, lakini kuna watu hawataki jambo hili kwa maslahi yao binafsi, nawashauri wabunge wasifuate mkumbo kwa mambo wasiyoyajua msukumo wake, kuna watu wanalipwa kwa jambo hili,” alisema Rage.

Tundu Lissu ashangaa Lakini akizungumzia tuhuma hizo katika viwanja vya Bunge jana, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alisema jambo hilo haliwezekani na ni kichekesho.

“Leo kampuni za mafuta zinunue wabunge wa upinzani ambao hawazidi 100, halafu iache wa CCM zaidi ya 260, maana nao hawautaki. Hakuna suala la kutumika na wafanyabiashara, hapa ni suala la muda huu si mwafaka kujadili miswaada hii. “Wabunge asilimia kubwa hatuitaki hii miswada, isipokuwa nilichoambiwa ni kuwa serikali inapewa presha na wafadhili ili iweze kupata fedha na kama wasipowasilisha bungeni miswaada hiyo hawatazipata,” alisema Lissu.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana mchana kwenye viwanja hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema ni kichekesho kutaka miswaada hiyo iahirishwe kwa kisingizo cha muda hautoshi.

“Nawaambia tusipopitisha sheria sasa itakuwa hasara kubwa kwa Watanzania, maana wanasema tusubiri Bunge lijalo, lakini hatuna uhakika na uwezo wa wabunge hao katika jambo hili, hivyo itabidi nao tuwajengee uwezo kama wa Bunge la sasa. “Wabunge hawa wamejengewa uwezo wameenda nchi mbalimbali kujifunza masuala ya gesi na mafuta na tangu mwaka 2010 tumeanza mchakato wa jambo hili, ndiyo sababu tunataka itungwe sasa vinginevvyo itakuwa matatizo mbele,” alisema Simbachawene.

Alisema hakuna msukumo wowote wa wafadhili ambao Serikali inaupata zaidi ya maslahi ya Watanzania na kusisitiza kuwa masuala ya kujadili mikataba na kampuni za gesi inachukua kati ya mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu, hivyo kama sheria mpaka mwakani itakuwa haijatungwa na uzalishaji umepangwa uwe kati ya mwaka 2018 na 2019 inamaanisha muda utazidi kusonga mbele na itakuwa hasara kwa Watanzania.

“Suala la majadiliano ya mkataba si la wiki moja au mwezi, ni kati ya mwaka mmoja na zaidi, sasa unasema Bunge lijalo ndiyo lifanye kazi hiyo unajua litakuwaje?

“Unasema watu mawazo yao yapo majimboni, hapa tatizo ni uvivu na kutojiandaa kwa baadhi ya wabunge majimboni ndiyo wanataka kuchangia miswaada isiwasilishwe,” alisema, lakini akikataa kuzungumzia kama baadhi ya wabunge wa upinzani wanatumiwa kukwamisha miswaada hiyo.

Pia alisema miswaada hiyo sio mipya badala yake imepitia hatua zinazotakiwa, ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuifanyia kazi na kuchukua maoni ya wabunge na wadau mbalimbali katika kuiboresha na wamesaidia kwa kiasi kikubwa.

Alisema pamoja na mambo mengine Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji ukipitishwa utafanya mikataba yote ya madini na gesi iwe wazi na halitakuwa jambo la siri kama ilivyo sasa.

Pia alisema ushiriki wa Watanzania lazima uwe wazi ijulikane wameshiriki kwa kiasi gani tofauti na sasa na kwamba pia gharama za uwekezaji na uzalishaji nazo zinatakiwa kuwa wazi, mambo ambayo ndiyo sababu wanataka yaharakishe miswada hiyo.

Alisema sheria italazimisha kujua taarifa kuhusu uwekezaji kama ni halisi na sahihi na kwamba hilo ni jambo muhimu na ndiyo sababu wanataka uwazi uwe katika sheria “Wanaoenda kufanya majadiliano ya kuingia mikataba sio wabunge ni wataalam, ndiyo sababu tunataka kuwapa nguvu za kisheria,” alisema Simbachawene. Imeandikwa na Amir Mhando na Namsembaeli Mduma.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company