Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) akifurahia jambo na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho walipohudhuria kikao cha dharura katika Hoteli ya Bahari Beach, jijini Dar es Salaam jana. kuanzia kushoto ni Ezekia Wenje, Mchungaji Peter Msigwa na Naibu Katibu wa chama hicho (Zanzibar), Salum Mwalimu. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Licha ya Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) kupokea taarifa ya Ukawa na kuamua chama hicho kiendelee kushiriki katika umoja huo, bado suala la mgombea urais wa vyama vinavyounda umoja huo limeendelea kuwa siri nzito.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya CUF jana, zilisema kuwa katika kikao chake kilichoketi juzi na jana mjini Zanzibar, baraza hilo lilipokea taarifa ya Ukawa, kuithibitisha na kuamua chama hicho kiendelee na ushirikiano huo.
Mkutano wa waandishi wafutwa
Pamoja na hayo, jana kutwa nzima viongozi wa Ukawa walikuwa kwenye vikao mfululizo na hakukuwa na taarifa rasmi zilizopatikana na hata mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa jana jioni uliahirishwa bila kueleza utaitishwa tena lini.(P.T)
Ingawa taarifa ya mkutano wa Ukawa na wanahabari haikutaja ajenda, habari zilizoenea katika mitandao ya kijamii zilibainisha kuwa walikuwa wanakusudia ama kutangaza chama kilichopitishwa na Ukawa kusimamisha mgombea urais au kutangaza jina la mgombea mwenyewe pamoja na mgombea mwenza.
Vyanzo mbalimbali ndani ya Ukawa, vilieleza kuwa ufunguo wa hatua hiyo ulikuwa unashikiliwa na CUF, ambayo hivi karibuni ilijitenga na umoja huo ili masuala yake yajadiliwe kwanza na vikao vyake vya maamuzi kabla ya kurejea kwenye meza ya majadiliano.
Taarifa za uhakika kutoka katika kikao hicho kilichoketi Zanzibar kwa siku mbili, zilibainisha kuwa wajumbe waliafikiana kinyume na ilivyotarajiwa kuwa wangevurugana.
Miongoni mwa mambo ambayo inadaiwa wameafikiana ni kuwa mgombea urais atoke Chadema na chama hicho kitoe mgombea mwenza.
Jussa: Watanzania mtafurahi
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Jussa Ismail Ladhu alipoulizwa alisema ikiwa itaamuliwa mgombea mwenza wa Ukawa atoke CUF, hakutakuwa na shida kwa kuwa chama hicho kina wanasiasa wazuri, safi na makini na kwamba kitatoa mtu ambaye Watanzania wote watafurahi.
“Ikiamuliwa kuwa mgombea mwenza atoke CUF, wananchi msiwe na wasiwasi, CUF ina hazina nyingi, itatoa mtu bora, itawapa chaguo ambalo Watanzania wote wataridhika nalo,” alisema Jussa.
Pamoja na kuthibitisha kuwa Baraza hilo limeamua CUF iendelee kushiriki katika umoja huo, Jussa alisema kwenye mjadala matatizo kidogo yalikuwapo katika mgawanyo wa majimbo.
Hata hivyo alisema baada ya kuweka vigezo vya kuwa na mgombea wa Ukawa, sasa hakuna shida kwa kuwa majimbo machache yaliyosalia utaratibu wake utatangazwa hivi karibuni.
Kuhusu mgombea mwenza, Jussa alisema CUF ina nafasi kubwa ya kutoa mgombea huyo kwa sababu ndicho chama chenye nguvu Zanzibar na kina wanasiasa mahiri na makini.
Wagombea wetu tunataka wawe ni wale watakaohakikisha kuwa Katiba Mpya inapatikana mara baada ya uchaguzi ili kuyaweka sawa mambo yanayohitaji kuwekwa sawa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba, mgombea urais na mgombea mwenza wanapaswa kutoka chama kimoja, hivyo kama Chadema itamtoa mgombea urais inabidi pia mgombea mwenza atoke chama hicho.
Habari ambazo bado si rasmi zinasema kuwa mmoja wa viongozi wa CUF anaweza kuhamia Chadema ili kukidhi matakwa hayo ya Katiba.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema kuwa mambo katika Ukawa ni mazuri, wapo waliofikiri kuwa watavurugana, lakini wamekubaliana na sasa Watanzania wasubiri kupata wagombea safi katika ngazi zote.
Bimani alisema CUF kitaendelea kushirikiana na vyama vingine vya upinzani nchini ili kuhakikisha demokrasia inazidi kukua.
Vikao mfululizo Chadema
Habari zaidi zilizolifikia gazeti hili zilisema mshirika mwingine wa Ukawa, Chadema jana viongozi wake walikuwa katika kikao cha dharura cha Kamati Kuu kilichoshirikisha wajumbe wachache, hasa wale wanaopatikana kwa kupigiwa kura ili kuweka mambo sawa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alikiri kuwapo kwa kikao hicho.
“Kamati Kuu ya Chadema inaendelea kukutana jijini Dar es Salaam kwa kikao maalumu cha dharura kujadili mambo mbalimbali,” alisema Makene katika taarifa yake fupi aliyotuma jana usiku.
“Mambo hayo ni pamoja na maandalizi ya chama kuelekea uchaguzi mkuu, kupokea taarifa za mwenendo wa kura za maoni na uteuzi wa awali wa nafasi za ubunge wa majimbo na viti maalumu zinazoendelea nchini nzima,” alisema Makene.
Habari za ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, zilisema kuwa kilikuwa na jukumu la kupokea taarifa ya utafiti iliyofanywa nchini kote kuhusu mgombea anayekubalika zaidi.
Ingawa hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu utafiti huo, lakini taarifa zinazoendelea kusambaa zinalitaja jina la waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa yuko mbioni kuhama chama chake cha CCM na kwenda Chadema, huku mgombea mwenza akitajwa kuwa atatoka upande wa Zanzibar CUF.
Mgombea mwenza kuhamia Chadema
Habari za ndani ya Ukawa zinasema chini ya makubaliano ya Ukawa ikiwa mgombea urais atatoka Chadema, mgombea mwenza akitoka chama kingine itabidi ahame chama chake ili aingie chama alicho mgombea urais ili kukidhi matakwa ya kikatiba.
“Tutakaposhinda uchaguzi, kama makamu wa rais atatoka CUF itabidi kila akitoka katika ofisi ya makamu wa rais, kituo cha kwanza atasimama Makao Makuu ya CUF kwa ajili ya kupeleka taarifa na kupata baraka za chama katika masuala muhimu.”
Chanzo chetu cha habari kinasema: “Ikiwa Ukawa tutashinda Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 na kupata nafasi ya urais, jambo la kwanza litakuwa ni kufanya Mabadiliko ya Katiba na kuruhusu demokrasia pana ya watu kuungana.”
Alisema hakuna ajabu yoyote kwa rais kutoka chama kimoja na makamu wa rais kutoka chama kingine.
“Hilo hata sasa linatendeka Zanzibar ambako Rais na Makamu wa Kwanza wa Rais wanatoka vyama tofauti na hakuna matatizo yoyote katika utendaji wa Serikali, kila mmoja anasimamia kwanza maslahi ya Taifa pili kuhakikisha sera za chama chake zinatekelezwa,” kilieleza chanzo cha habari.
Lowassa atajwa
Hii ndiyo ajenda ambayo imetawala mijadala kuhusu fununu za Lowassa kuhama CCM kwenda Chadema ili kukamilisha safari yake ya matumaini.
Gazeti hili linafahamu kuwa mazungumzo na Lowassa yamekwishafikia hatua nzuri ingawa kulikuwa na viongozi wachache ndani ya Chadema waliokuwa wameshikilia msimamo wa kumkataa lakini kutokana na presha iliyopo ndani na nje ya chama wasingefua dafu.
Mtei amkaribisha
Huku mjadala kuhusu Lowassa ukizidi kukolea, mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei amemkaribisha mwanasiasa huyo na makada wengine wa CCM kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mtei alisema kwa sasa Chadema na Ukawa wanahitaji kura za kutosha kuing’oa CCM, hivyo hata kura ya mtu mmoja ni muhimu.
“Nimesikia Lowassa anatajwa kutaka kujiunga na Chadema, mimi namkaribisha aje, si yeye tu, aje na makada wengine wa CCM kwa kuwa tunapaswa kuimarisha nguvu za kuiondoa CCM madarakani,” alisema.
Alisema Chadema ni chama cha Watanzania wote hivyo hakiwezi kumfungia milango Mtanzania mwenye sifa za kujiunga na chama hicho asijiunge.
Hata hivyo, Mtei alisema makada hao wa CCM ambao wanataka kujiunga na Chadema endapo watakuwa na nia ya kupata uongozi, wajue kuna vikao vya kuwapitisha.
“Tunawakaribisha Chadema makada wote wa CCM bila masharti na kama wana nia ya uongozi Chadema ina vikao vya kupitia kulingana na sifa zao na vikao vitakuwa na maamuzi ya mwisho,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, alisema ana uhakika muungano wa upinzani ndio silaha kubwa ya kuing’oa CCM madarakani.
“Uchaguzi uliopita Chadema tulishinda lakini tulichakachukuliwa lakini safari hii kupitia Ukawa tumejipanga kuhakikisha upinzani tunashinda kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Alisema hadi sasa Chadema na ukawa kwa ujumla wake kuna viongozi wenye sifa ya kushinda urais na wanakubalika nchi nzima.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago