SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, kukiri kupumzika kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Wilbrod Slaa, baadhi ya wasomi wamedai huo ndiyo mwanzo wa kupasuka kwa CHADEMA.
Walisema mpasuko huo pia utavihusisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), wameushutumu uongozi wa chama hicho kubariki Bw. Juma Duni Haji kujivua uanachama wa CUF kujiunga na CHADEMA.
Walimshutumu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kukubali uamuzi wa kumtoa Bw. Haji na kukisaliti chama chake.
Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini, wametoa maoni yao wakisema Dkt. Slaa ni kati ya viongozi wa CHADEMA ambao walitumia muda wao mwingi kukijenga chama hicho; pia ana kundi kubwa la watu wanaomwamini, hivyo kuondoka kwake ni pigo kwa chama hicho.
Wachambuzi hao walisisitiza kuwa, suala la kupumzika Dkt. Slaa katika kipindi hiki limegubikwa na sintofahamu; hivyo ni wazi kuwa wapo baadhi ya wanachama wanaoweza kukihama chama hicho.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Benson Bana, alisema viongozi wa CHADEMA watajifunza baada ya ndoto yao ya kushika dola kukwama akidai wamefanya maamuzi ya haraka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dkt. Andrew Swai, alisema kitendo cha Bw. Lowassa kwenda CHADEMA, kitaitikisa CCM, CHADEMA na UKAWA akiamini Bw. Lowassa ataingia na kundi kubwa la watu ambapo pia Dkt. Slaa ataondoka nao.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHR), Dkt. Hellen Kijo Bisimba, alisema ni mtikisiko mkubwa ndani ya vyama lakini ndivyo siasa ilivyo.
Alisema siasa za Tanzania hazitabiriki ambapo Dkt. Slaa ana watu wengi pamoja na Bw. Lowassa; hivyo ndani ya vyama vyote ni mtikisiko hakuna chenye nafuu zaidi ya kingine.
Wasomi wengine ambao hawakutaka majina yao yaandikwe walisema Bw. Lowassa amefanya maamuzi sahihi kuhamia CHADEMA na viongozi wa chama hicho wamejiridhisha kuwa kiongozi huyo ni mtu makini anayekubalika na Watanzania wengi.
Walisema hakuna mpasuko unaoweza kutokea ndani ya CHADEMA na UKAWA kwani viongozi wote wanaounda umoja huo walifanya utafiti wa kutosha kabla ya kumpokea Bw. Lowassa na kumbariki kuwa mgombea urais kupitia umoja huo.
Waliongeza kuwa, Bw. Lowassa ametumia haki yake ya kidemokrasia kuhamia CHADEMA na si mwanachama wa kwanza kutoka CCM na kuhamia vyama vingine vya upinzani.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago