Chadema waingia na ajenda ya CCM bungeni



Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika (katikati) akizungumza na aliyekuwa Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat), Dk Rodrick Kabangila, baada ya kutangaza kujivua nafasi za uongozi ndani ya chama hicho na kujiunga na Chadema Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Naomi Kaiula. Picha na Fidelis Felix
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Siku 12 baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwataja mawaziri watatu kuwa wameshindwa kuwajibika na kutaka wahojiwe na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Chadema kimeibuka na kusema kitaanika utendaji mbovu wa viongozi hao katika mkutano wa Bunge unaoanza kesho Mjini Dodoma.

Ili kufanikisha mkakati wake, chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kimewaomba wabunge wa CCM kuwapa ushirikiano katika mkakati wake wa kuwawajibisha mawaziri hao.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika aliwataja mawaziri hao kuwa ni wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.


Mnyika alisema Chadema kimefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa mawaziri hao wameshindwa kusimamia wizara zao kikamilifu.


Aidha, hatua hiyo imekuja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kukaririwa akilalamikia utendaji mbovu wa baadhi ya mawaziri hao.


Nape alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akiwataja Chiza, Malima na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa na alimsafisha Dk Kawambwa na kudai kuwa hakupaswa kuhusishwa na utendaji mbovu wa Kampuni ya Progressive iliyokuwa imepewa kazi ya kujenga Barabara ya Namtumbo-Tunduru.


Aliwashukia Chizza na Malima kwa kushindwa kufika mkoani Ruvuma kusikiliza kero za wakulima ambao alisema wanakabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwamo ya pembejeo.


Katika maelezo yake ya jana, Mnyika amemwongeza Profesa Muhongo na kusema Chadema kitawatumia mawaziri wake vivuli wa Wizara za Nishati, Kilimo na Elimu kuwasilisha udhaifu wa kiutendaji wa mawaziri hao.


Mnyika alisema uamuzi huo umekuja baada ya chama hicho kuzindua rasimu ya Sera ya Mabadiliko na Tabianchi ambayo inasisitiza kuwa mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na Serikali kushindwa kusimamia vizuri sekta ya nishati na madini, mifugo na kilimo.


“Inatakiwa suala la mabadiliko ya tabianchi liingizwe katika mfumo wa elimu yetu ikiwa ni pamoja na wananchi kuelimishwa. Katika kilimo na mifugo kuna tatizo kubwa kwani ardhi inatumika vibaya na kusababisha mabadiliko makubwa ya tabianchi lakini mawaziri na Serikali yao wapo kimya,” alisema Mnyika na kuongeza:


“Tunawaomba wabunge wa CCM watuunge mkono wakati Chadema tutakapoanza kuwashughulikia mawaziri hawa. Wabunge hawa wanatakiwa kudhihirisha kuwa wana uchungu na wasishindwe kama ambavyo wameshindwa kushughulikia ufisadi na rushwa ndani ya chama chao.”


Mnyika alisema ni aibu kwa Kinana kuwataka mawaziri kuwajibishwa halafu Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akakaa kimya bila kuchukua hatua yoyote... “Tunataka Rais Kikwete aseme chochote katika hili. Jambo la kuwang’oa mawaziri hawa si la kuzungumzwa jukwaani, linatakiwa kuletwa bungeni kwa sababu Bunge ndicho chombo kinachoweza kuibana vilivyo Serikali.”


Kuhusu rasimu hiyo, alisema Chadema kimeitoa ili kuwapa wananchi fursa ya kutoa maoni yao kazi ambayo itakamilika Desemba 31, mwaka huu kabla ya kuanza kuandaa mchakato wa kutoa sera.


Alisema kwa muda mrefu viongozi wa Serikali wamekuwa wakihudhuria makongamano mbalimbali ya tabianchi, lakini wameshindwa kumaliza tatizo la uwepo wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuweka mikakati ya nchi kutumia nishati mbadala ili kupunguza hewa hiyo.


“Mafuriko, ukame, vyanzo vya maji kutoweka, mgawo wa umeme ni baadhi ya matatizo yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, tusipokuwa makini kumaliza tatizo hili tutaangamia,” alisema.


Mnyika alisema katika rasimu hiyo kuna masuala ya Kikatiba ambayo yatajadiliwa baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa Rasimu ya pili ya Katiba: “Tunasubiri kuona rasimu itaeleza nini kuhusu suala la nishati na madini, elimu na mifugo na kilimo ili tuongeze katika sera hii.”
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company