Polisi ya Nigeria imetangaza kuwa, idadi ya wanafunzi wa kike waliotekwa nyara na waliopotea nchini humo, imeongezeka na kufikia 276. Kwa mujibu wa polisi, idadi hiyo imeongezeka baada ya wanafunzi wengine 30 kuripotiwa kupotea hivi karibuni. Hayo yanajiri katika hali ambayo kwa mujibu wa habari, idadi rasmi ya wanafunzi wa kike waliotekwa nyara na wanachama wa kundi la Boko Haram hapo tarehe 14 mwezi jana inatajwa kuwa 300. Kwa upande mwingine kiongozi mmoja wa polisi amenukuliwa akisema kuwa, idadi ya mabinti na wasichana ambao wamefanikiwa kutoroka kutoka mikononi mwa wanachama hao wa Boko Haram imeongezeka na kufikia 53. Hayo yanajiri katika hali ambayo hapo jana maelfu ya raia wa Nigeria waliandamana kulalamikia udhaifu wa serikali katika juhudi za kuwaokoa wasichana hao waliotekwa nyara na wanachama wa Boko Haram. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, wanachama wa kundi hilo wanapinga mafundisho yenye kufuata mfumo wa kisekula hususan kwa wasichana, huku wakitekeleza mashambulizi dhidi ya shule za mabweni za wanafunzi hao.