Polisi Nigeria:Waomba picha za wanafunzi


Waandamanaji nchini Nigeria wakidai wasichana waliotekwa katika mji wa Chibok, Borno warejeshwe

Polisi nchini Nigeria wamewataka wazazi wa wanafunzi wasichana zaidi ya 200 waliotekwa kuwasilisha picha za mabinti hao.

Wasichana hao walichukuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kiislam kutoka shuleni kwao katika jimbo la Borno zaidi ya wiki mbili zilizopita.
Polisi wa jimbo la Borno wameiambia BBC kuwa serikali inataka kuthibitisha bayana ni nani ambaye ametoweka kwa sababu vitabu vya kumbukumbu vya shule vilichomwa moto katika shambulio hilo.

Waandamanaji wengine wakitaka rais wa Nigeria asaidie kuwaokoa wasichana waliotekwa jimbo la Borno

Polisi wamesema kwa sasa inafikiriwa kuwa wasichana wapatao 223 bado hawajulikani walipo.

Maandamano yalifanyika siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi, ambayo ni mapumziko, waandamanaji wakitaka hatua zaidi zichukuliwe kuwaokoa wanafunzi hao wa kike.

Kundi la Kiislam la Boko Haram halijatamka lolote kuhusiana na tuhuma zinazolikabili kuwa wapiganaji wake wamehusika na utekaji wa wanafunzi hao kutoka shuleni kwao katika mji wa Chibok usiku wa manane wa tarehe 14 Aprili 2014.

Kundi hilo, ambalo jina lake lina maana ya "Elimu ya mgaharibi ni haramu" katika lugha ya Kihausa, limekuwa likiendesha mashambulio mbalimbali kaskazini mwa Nigeria katika miaka ya hivi karibuni, huku watu 1,500 wakikadiriwa kuuawa katika ghasia hizo na msako wa vyombo vya usalama mwaka huu pekee.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company