WATIA nia wanne waliochukua fomu za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wagombea wa kiti cha urais wametupwa nje ya mchakato huo, baada ya kushindwa kurudisha fomu.
Walioshindwa kurudisha fomu hizo mpaka muda wa mwisho ulipofika saa 10.00 jioni jana ni Peter Nyalali, Helena Elinewinga, Anthony Chalamila na Dk Muzamil Kalokola.
Mmoja wa watia nia hao, Helena mara baada ya kuchukua fomu Juni 25, mwaka huu, alikwenda kumtembelea mmoja wa maofisa wa chama hicho akitafuta ushauri wa namna ya kufanya ili kupata udhamini, lakini baadaye aliamua kutelekeza fomu hizo bila kuondoka nazo.
Jumla ya wanachama 42 walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba uteuzi huo ambapo walitakiwa kuwa na wadhamini 450 kutoka mikoa 15, ikiwemo mitatu ya Zanzibar.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rajab Luhwavi alisema zoezi la kuchukua fomu lilianza Juni 3, mwaka huu na lilitarajia kumalizika Julai 2 saa 10.00 jioni.
Alisema zoezi hilo limefanyika kwa utulivu ambapo kati ya wanachama 42 waliochukua fomu na kutakiwa kuwa na wadhamini kutoka mikoa 15 ikiwemo mitatu ya Zanzibar ambapo kati ya hao ni 38 ndio waliofanikiwa kurejesha fomu.
Alisema hatua itakayofuata ni mchakato wa vikao vya chama kuanzia Jumanne wiki ijayo.
“Mmoja wa wachukua fomu, Helena Elinawinga alitelekeza fomu hizo kwa mmoja wa maofisa wa CCM baada ya kufika kuomba ushauri huku akitaka kupewa kwanza elimu ya siasa kabla ya kuanza kutafuta wadhamini,” alisema Luhwavi.
Sita warejesha fomu
Wakati makada wanne washindwa kurejesha fomu hizo, wenzao sita waliwahi muda uliowekwa wa kurejesha fomu na wakawa na sifa za kujadiliwa na vikao vya maamuzi.
Ngeleja na mambo 15
Wa kwanza kurudisha fomu hizo alikuwa ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ambaye aliendelea kusisitiza kuwa CCM wamtafakari kwa mambo 15 aliyoyafanya wakati akiwa waziri wa nishati na madini.
Ngeleja, ambaye alirudisha fomu saa 4.45 asubuhi ambaye hata hivyo hakutaja mambo hayo 15, alisema yeye ni kiongozi makini na Watanzania hawatajuta ikiwa atachaguliwa kuongoza nchi.
“Nina maono ya ndoto, CCM ni chama kikongwe ndoto zangu si za mchana ninayoyatafakari tayari yamefanyika nchi nyingi duniani,” alisema.
Alisema taifa limekuwa likijengwa na makundi ya wafanyakazi, wakulima na wafugaji ambapo makundi hayo uanabena taswira nzima na kama taifa linatakiwa kupiga vita umaskini, maradhi na ujinga.
Alisema ni lazima kuendeleza juhudi zinazofanywa na wajasiriamali na wanamichezo pamoja na wasanii kwani ni kundi kubwa na limekuwa likiingiza kipato kutokana na shughuli wanazofanya.
“Iwapo nitachaguliwa nitaendeleza sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi,” alisema. Alisema kilimo kimebeba Watanzania asilimia 75 na kama taifa ni muhimu kuwekeza kwenye kilimo na kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua na badala yake kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Balozi Patrick Chokala
Patrick Chokala alirudisha fomu saa 11.29 jioni na kusema kitendo chake cha kuchukua fomu na kukamilisha kutafuta wadhamini ni kuwa amedhamiria na ana uwezo wa kuongoza serikali ana uzoefu na hakuna geni kwake.
Pia ana uwezo wa kuendeleza uhusiano wake wa kimataifa kwani elimu yake ni ya chuo kikuu na kama rais wa Tanzania atadumisha umoja na ushirikiano hatayumbishwa na mtu yeyote yule na kuondoka katika misingi ya Watanzania.
“Sina hulka ya udikteta na ufashisti na wananchi wasiwe na wasiwasi wataendelea kwa umoja,” alisema. Pia atakuwa mtetezi wa wanyonge kwani chama hicho ni cha wakulima na wafanyakazi na ataangalia watu wa chini.
Alisema ni viongozi wajinga wanasisitizia mambo yasiyo ya lazima na kusahau kule chini kwenye kiatu. Alisema ana ujasiri mkubwa wa kupambana na udhalimu kwa wananchi.
“Mimi ninastahili kuwa Rais wa nchi kwani nina uwezo na uzoefu wa kuongoza serikali, pia kuendeleza ushirikiano wa kimataifa,” alisema. Alisema atadumisha umoja na kwamba hatayumbishwa na yoyote katika masuala ya msingi.
Banda Sonoko
Sonoko yeye alirejesha fomu na kusema kuwa fomu moja ya mkoa wa Iringa haijafika na kama itafika kabla ya saa 10 atairejesha.
Alisema kutafuta wadhamini kulimpa wakati mgumu juu ya namna ya mawasiliano na kukusanya wanachama kwa ajili ya kuwatoa na kuwapeleka kwenye ofisi za chama.
Alisema akipata nafasi ya kuwa rais wa nchi hatotoa kipaumbele kwa nchi kuendeshwa kwa fedha za wahisani na pia atatoa uhuru wa habari ili jamii ijengeke kiuelewa. Pia alisema ataendeleza mazuri ya Jeshi la Magereza kwa kupunguza idadi kubwa ya wafungwa.
“Nitaanzisha magereza mbadala ya wafungwa nyumbani ambapo watakuea wakiripoti serikali za mitaa kila siku na kufanya shughuli za kijamii katika maeneo ya jirani, wateja wa magereza watakuwa watu wenye mashauri ya jinai,” alisema.
Kwa upande wa elimu alisema ataanzisha shule ya mfano itakayoanzia chekechea hadi chuo kikuu na kwamba itakuwa na masomo matatu ya kiswahili, uraia na utaalamu wa hesabu ili nchi ipate wataalamu waliobobea.
Godwin Mwapongo
Kwa upande wake, Mwapongo alisema amekamilisha mikoa yote 15 na hakuombwa chochote wakati wa kutafuta wadhamini mikoani.
Alisema atapambana na rushwa kwa kuwarudishia wananchi madaraka na hivyo wataweza kupambana na rushwa uso kwa uso. Alisema lazima mamlaka yarudishwe kwa wananchi ili wawe na uwezo wa kudhibiti rushwa.
Alisema iwapo atachaguliwa atarudisha Azimio la Arusha, lakini si kwa ajili ya kunyang’anya mali za watu, lakini mali ambayo haikupatikana kwa njia zisizo sahihi si baraka.
Alisema wale ambao walinyang’anywa wakati huo ambao bado wako watarudishiwa mali zao. Alisema akiwa Rais hatakubali kuwa Mwenyekiti wa CCM kwani kuwa na kofia mbili hakuna nafasi za kuhoji.
Ritha Ngowi
Ngowi kwa upande wake CCM ilimpa ushirikiano na hivyo kumwezesha kupata wadhamini bila tatizo lolote. Alisema maeneo mengine walijitokeza kwa wingi, jambo ambalo lilimpa moyo sana.
Ngowi alisema alizunguka mikoa 15 na ametimiza yote aliyotakiwa kutimiza.
January Makamba
Makamba yeye amekitaka chama chake, kuteua mgombea atakayewakilisha chama hicho kwa nafasi ya urais kwa kuzingatia busara za waasisi wa chama hicho, akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Amesisitiza kuwa Watanzania na wanachama wa chama hicho wanataka wagombea wa CCM kwa nafasi za ngazi zote ambao wana mvuto kwa watu na ambao itakuwa rahisi kuwanadi bila kuwatolea maelezo au utetezi kwanza.
January aliyasema hayo, mjini Dodoma, mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kutafuta wadhamini katika baadhi ya mikoa nchini pamoja na kurejesha fomu ya kuomba kugombea Urais kupitia chama hicho tawala.
Alisema mwaka 1995, Mwalimu Nyerere wakati akihutubia mkutano mkuu wa chama hicho wa kumteua mgombea Urais wa CCM, alisema kwamba, “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM”.
Aidha alisema naye Mwenyekiti na Rais mstaafu wa chama hicho, Benjamin Mkapa, wakati akihutubia mkutano mkuu wa CCM wa kumteua mgombea Urais wa CCM mwaka 2005, alisema ni muhimu CCM ikatazama aina ya wapiga kura waliopo, ambao wengi ni vijana, na kuwapatia mgombea anayeendana nao.
“Miaka 20 baadaye, kauli ile ya Mwalimu na miaka 10 baadaye kauli ya Mkapa bado ziko sahihi. Katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM inayo nafasi ya kuwapa Watanzania aina ya mgombea anayeashiria na kuakisi mabadiliko wanayoyataka watanzania,” alisisitiza.
Alisema ana imani kuwa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho, utazingatia busara hizo za zilizofanya chama hicho, kupata wagombea sahihi mwaka 1995 na 2005.
“Nina imani kubwa na viongozi wakuu wa chama chetu katika kutuongoza kupata mgombea anayeakisi hadhi, heshima na dhamana ya chama chetu,” alisema.
Alisema pia Rais na Mwenyekiti mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alipata kusema, “kila zama na kitabu chake”. Na kusisitiza kuwa umri sio sifa ya uongozi lakini uongozi unaenda kwa rika au kizazi.
Alisema kila kizazi kina wakati wake, kila zama zina changamoto na mahitaji yake na kila kizazi kina wajibu mahsusi wa kukabiliana na changamoto za wakati wake.
“Vizazi vilivyopita vya viongozi wetu vimeiongoza nchi yetu vizuri na mafanikio yako dhahiri. Baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru, sasa ni wakati wa kizazi kingine kitakachokuja na fikra mpya, mtazamo mpya na majawabu mapya kwa changamoto za sasa,” alisisitiza.
Kwa upande wake, alisema ameshapima na kujitafakari na anaamini ameandaliwa vizuri kiuongozi na kimaadili kwenye chama, Serikali, bungeni katika utumishi wake Ikulu.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago