Dk Asha-Rose Migiro PICHA|MAKTABA
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam.Rais Jakaya Kikwete amemteua Dk Asha-Rose Migiro kuwa Mbunge.
Uteuzi huo unamrejesha Dk Migiro bungeni baada ya kuondoka Januari 5, 2007 akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na kuhudumu hadi alipomaliza muda wake Januari mwaka jana.
Baada ya kurejea nchini, Dk Migiro aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais jana, ilimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Florens Turuka akisema uteuzi huo umeanza tangu juzi.
Uteuzi huo unatokana na mamlaka ya kikatiba aliyo nayo Rais Kikwete ya kuteua wabunge 10.Mwanasiasa huyo aliyezaliwa Julai 9, 1956, aliwahi pia kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuanzia mwaka 2000 hadi 2005.